1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Marekani yasitisha msaada wa dola milioni 500 kwa Niger

11 Oktoba 2023

Marekani imesitisha msaada wa zaidi ya dola milioni 500 kwa taifa hilo la Sahel linalokabiliwa na uasi wa makundi ya kigaidi huku msafara wa kwanza wa wanajeshi wa Ufaransa ukiwa umeondoka Niger siku ya Jumanne.

https://p.dw.com/p/4XORZ
Niger Niamey | Besuch US-Außenminister Anthony Blinken
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akisalimiana na aliyekuwa mwenzake wa Niger Hassoumi Massoudou (Niamey-Niger:16.03.2023).Picha: Boureima Hama/AP/picture alliance

Marekani imesitisha jana msaada wa zaidi ya dola milioni 500 kwa taifa hilo la Niger, na kutangaza kuwa jeshi la Niger lilifanya mapinduzi mnamo Julai 26, na kuiondoa madarakani serikali iliyochaguliwa kidemokrasia.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Matthew Miller, amesema kurudishwa kwa msaada wa nchi yake kwa Niger, kutahitaji kuchukuliwa kwa hatua za kurejesha uongozi wa kidemokrasia haraka iwezekanavyo.

Soma pia: Blinken azungumza na Bazoum kwa njia ya simu

Siku ya Jumatatu Marekani ilitoa wito wa kuachiliwa mara moja wale wote wanaozuiliwa kinyume cha sheria kufuatia mapinduzi hayo ya kijeshi. Hapo jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alifanya pia mazungumzo na rais aliyepinduliwa Mohamed Bazoum na kumhakikishia uungaji mkono kwa utawala uliochaguliwa kidemokrasia katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Msafara wa kwanza wa wanajeshi wa Ufaransa waondoka Niger

	Niger Niamey | Abdourahamane Tiani
Kiongozi mpya wa utawala wa kijeshi nchini Niger Jenerali Abdourahmane TianiPicha: Télé Sahel/AFP

Utawala wa kijeshi wa Niger umetangaza kwenye televisheni ya taifa jana usiku kwamba umeusindikiza msafara wa kwanza wa wanajeshi wa Ufaransa kutoka kambi waliokuwemo katika mji wa magharibi wa Ouallam na "kuelekea Chad".   

Kuondolewa kwa vikosi vya Ufaransa kuliamriwa haraka na majenerali walionyakua madaraka nchini  Niger  mnamo Julai 26, huku Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akithibitisha mwezi Septemba kuondoka kwao, mchakato ambao serikali ya Paris inatarajia kuukamilisha mwishoni mwa mwaka huu.

Takriban wanajeshi 1,000 wa Ufaransa walikuwa katika kambi mjini Niamey, huku wengine 400 wakiwekwa katika kambi mbili zilizopo kaskazini-magharibi, karibu na mipaka ya Mali na Burkina Faso, mahali kunakoripotiwa harakati mbalimbali za waasi.

Soma pia: Jeshi la Ufaransa laanza operesheni za kuondoka Niger

Niger Niamey Demo Putschisten Anhänger Anti Frankreich
Raia wa Niger wakiandamana mjini Niamey wakidhihirisha chuki dhidi ya Ufaransa (03.08.2023)Picha: Stringer/Reuters

Baadhi ya raia wa Niger wametaja kufurahishwa na hatua hiyo, Ali Hassane ni mkaazi wa mjini Niamey:

"Nakuhakikishia kwamba hivi ndivyo Wafaransa wanavyoondoka. Tunajivunia kwa sababu hapo mwanzoni hatukuamini jambo hili lingewezekana. Asante Mungu, shukrani kwa vikosi vyetu vya jeshi na kwa watu wa Niger. Hatimaye zoezi limeanza. Tunamshukuru Mungu.”  

Mbali na wanajeshi waliondoka kwa njia ya barabara, kulikuwepo pia safari tatu katika uwanja wa ndege huko Niamey, ambazo zimewasafirisha wanajeshi 97 wa vikosi maalum na wale wanaohusika na ukaguzi na usambazaji wa vifaa vya kijeshi.

Soma pia:Mkuu wa Jumuiya ya ECOWAS apendekeza kipindi cha miezi 9 nchini Niger 

Niger Französische Soldaten unterstützen französische Staatsangehörige auf einem Flugplatz
Wanajeshi wa Ufaransa wakiwalinda raia wa Ufaransa waliokuwa wakijiandaa na safari katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa NIamey: (01.08.2023)Picha: Sam Mednick/AP Photo/picture alliance

Marekani, Ufaransa ambao ni wakoloni wa zamani wa Niger, pamoja na Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi  ECOWAS,  wamekuwa wakiwashinikiza watawala wa kijeshi kumuachia huru na kumrejesha mamlakani Rais Mohamed Bazoum, matakwa yaliyotupiliwa mbali.

Afisa mwingine wa serikali ya Washington amesema Marekani bado ina jumla ya wanajeshi wapatao 1,000 nchini Niger, lakini kwa sasa hawatoi tena mafunzo au kuvisaidia vikosi vya Niger lakini wataendelea na shughuli za kufuatilia vitisho kutoka kwa makundi ya kigaidi.

Vyanzo: (afpe,rtre)