1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Niger: Tunatumaini kufikia makubaliano chanya na ECOWAS

Hawa Bihoga
5 Septemba 2023

Waziri mkuu alieteuliwa na utawala wa kijeshi nchini Niger Ali Mahaman Lamine Zeine amesema katika siku za usoni anaona matumaini ya kufikia makubaliano na jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS.

https://p.dw.com/p/4VyNK
Niger Ali Mahaman Lamine Zeine Interview
Waziri Mkuu wa Niger Ali Mahaman Lamine ZeinePicha: DW

Katika mkutano wake na waandishi wa habari waziri mkuu Ali Zeine amesema kwamba mawasiliano baina ya pande mbili yanaendelea, hii ni kutokana na kuondoka kwa haraka kwa vikosi vya Ufaransa vilivyokuwa nchini Niger, baada ya uhusiano na Ufgaransa kuzorota kufuatia jeshi kutwaa madaraka.

Amesema bado hawajasitisha mawasiliano na jumuiya ya ECOWAS na wanayo matumaini chanya katika kufikia makubaliano kwa siku zijazo.

"Tumepokea wajumbe mara nne, sisi wenyewe tumefanya ziara."

Aliongeza kwamba katika mfululizo wa mawasiliano unaoendelea wanayo matumaini kufikia makubaliano na hatimae kuondolewa kwa vikwazo.

Soma piaMaandamano ya kutaka wanajeshi wa Ufaransa waondoke yafanyika Niger:

"Tuna imani katika siku chache tutaweza kufikia makubaliano ili vikwazo hivi vyote viweze kuondolewa."

Akizungumzia masuala ya usalama amesema kuna kitisho cha kushambuliwa wakati wowote, lakini tayari wamechukua tahadhari za kiusalama ikiwemo kujilinda.

Vikwazo ya ECOWAS kwa Niger

ECOWAS imeiwekea Niger vikwazo vikali baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Julai yaliomuondoa madarakani rais aliechaguliwa kidemocrasia Mohamed Bazoum.

Mara kadhaa imekuwa ikitishia kuingilia Niger kijeshi ili kurejesha utawala wa Bazoum, ikiwa jitihada za kidiplomasia za kutatua mzozo huo hazitafua dafu.

Ufafanuzi:Kwanini Niger ni muhimu kwa mataifa ya magharibi?

Rais wa Nigeria Bola Tinubu ambaye pia ni mwenyekiti wa sasa wa ECOWAS siku ya Alhamisi iliyopita alipendekeza kipindi cha mpito cha miezi tisa, kama vile nchi yake ilivyopitia mwishoni mwa miaka ya 1990.

"Rais haoni sababu kwa nini hali kama hiyo haiwezi kuigwa nchini Niger, ikiwa mamlaka ya kijeshi ya Niger ni waaminifu," ofisi ya rais wa Nigeria ilisema katika taarifa.

Soma pia:Jumuiya ya ECCAS yaisimamisha uanachama Gabon
 Algeria, jirani mwenye ushawishi mkubwa wa kaskazini mwa Niger, imependekeza kipindi cha mpito cha miezi sita.

Watawala wa kijeshi nchini Niger hawajatoa tamko lolote kuhusu mapendekezo juu ya kipindi cha mpito.

ECOWAS imechukua msimamo mkali kuhusu Niger kufuatia msururu wa mapinduzi katika eneo lake tangu 2020.

 Wanajeshi wamechukua mamlaka nchini Mali na Burkina Faso, sawa na  Niger, mataifa yanyayokabiliwa na uasi wa muda mrefu wa wanajihadi.

Embalo afanya uteuzi kujihakikishia usalama

Rais wa Guiena -Bissau Umaro Sissoco Embalo amewateua maafisa wawili wapya kulinda usalama wake, ambao walianza majukumu yao hapo jana Jumatatu.

Rais huyo wa nchi amegusia kuhusu mapinduzi ya kijeshi kwingineko barani Afrika, katika hafla ya kuapa kwa maafisa hao wa usalama. 

Äthiopien | African Union Gipfel in Addis Ababa | Umaro Sissoco Embalo
Rais wa Guinea Bissau Umaro Sissoco EmbaloPicha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Uteuzi huo wa kiusalama ulifanyika muda mfupi baada ya mapinduzi nchini Niger na Gabon, yote yaliyofanywa na maafisa wa usalama wa serikali.

Jenerali Tomas Djassi aliteuliwa kuwa mkuu wa usalama wa rais, huku Jenerali Horta Inta akiteuliwa kuwa mkuu wa wafanyikazi wa rais siku ya Ijumaa, na kuapishwa Ikulu hapo jana.

Nafasi hizi mbili zimekuwepo kwa muda mrefu katika muundo wa shirika la serikali lakini hazijajazwa kwa miongo kadhaa.

Soma pia:ECOWAS kutuma ujumbe wa kijeshi nchini Guinea-Bissau

Guinea-Bissau imekumbwa na mapinduzi manne ya kijeshi tangu uhuru wake mwaka 1974, na hivi karibuni zaidi yakiwa ni mwaka 2012.

Jaribio la kumpindua Embalo lilifanyika mnamo Februari 2022, rais Embalo aliwaambia waandishi wa habari kwamba mapinduzi ya kijeshi yaliofanywa na maafisa usalama wa rais yamekuwa ni mtindo.

Ameonya kwamba "vuguvugu lolote linalotiliwa shaka litakabiliwa na jibu linalofaa".

Mwezi uliopita, Embalo alionya kwamba mapinduzi ya Niger yalileta tishio lililopo kwa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS, akisema rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum ndio kiongozi halali wa taifa hilo la Afrika magharibi.