1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

ECOWAS yapendekeza kipindi cha mpito cha miezi 9, Niger

Sylvia Mwehozi
1 Septemba 2023

Rais wa Nigeria Bola Tinubu aliye pia mkuu wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, amependekeza kipindi cha mpito cha miezi tisa hadi kurejea kwenye demokrasia nchini Niger.

https://p.dw.com/p/4Vpix
Nigeria Abuja | ECOWAS-Treffen zu Niger-Putsch
Picha: Gbemiga Olamikan/AP/picture alliance

Hilo ni pendekezo la kwanza la kuwepo kipindi cha mpito nchini Niger kutoka jumuiya ya ECOWAS  tangu wanajeshi walipoipindua serikali Julai, 26. Jumuiya hiyo ya kikanda imeiwekea Niger vikwazo baada ya wanajeshi kumuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum na imetishia kuingilia kati kijeshi iwapo mazungumzo ya kurejesha utawala wa kiraia yatashindikana.

Tinubu amesema hakutakuwa na msamaha wa kuviondoa vikwazo vilivyowekwa na ECOWAS hadi serikali ya  Niger  ifanye marekebisho chanya. Kupinduliwa kwa serikali ya Niger kumezua wasiwasi katika nchi zote za Afrika Magharibi ambapo, tangu mwaka 2020, serikali za Mali, Guinea na Burkina Faso  zimepinduliwa na wanajeshi.

Hofu imeongezeka zaidi kutokana na uasi wa jeshi mnamo wiki hii nchini Gabon ambapo Rais Ali Bongo, alipinduliwa muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi mwishoni mwa juma lililopita.