1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuchagua rais mpya leo

3 Novemba 2020

Raia wa Marekani wanapiga kura leo (03.11.2020) kumchagua rais mpya kati ya Donald Trump wa Republican anayewania muhula wa pili au mpinzani wake wa chama cha Democratic ambaye pia ni makamu wa rais wa zamani, Joe Biden.

https://p.dw.com/p/3kmth
USA Wisconsin | Wahlkampf | Joe Biden Anhänger
Picha: Bing Guan/Reuters

Hadi jana Jumatatu, Biden alikuwa mbele ya Trump kwenye kura za maoni ya umma kuelekea uchaguzi wa leo unaofanyika chini ya kiwingu cha janga la virusi vya corona ambalo limewauwa mamia kwa maelfu ya watu nchini Marekani.

Trump, rais wa 45 wa Marekani anajivunia rikodi ya kuimarisha uchumi na kupunguza kwa kiwango kikubwa ukosefu wa ajira lakini anakosolewa kwa jinsi alivyoshughulikia janga la virusi vya corona.

Biden, mwanasiasa anayegemea sera za wastani za mrengo wa shoto ameahidi kulinda haki ya wamarekani kupata huduma za afya, mafao kwa wazee na kutengeneza nafasi mpya za kazi kupitia sekta ya nishati jadidifu.

Mchuano ni mkali na wasiwasi umetanda juu ya kuzuka mabishano baada ya uchaguzi huu, baada ya Rais Trump kutishia kujitangazia ushindi hata kabla ya matokeo kukamilika. 

Wagombea hao wachuana majimboni 

USA Präsidentschaftswahl 2020
Picha: Go Nakamura/Reuters

Saa chache kabla ya kufunguliwa vituo vya kupigia kura katika siku ya uchaguzi wa Marekani unaofanyika leo, rais Donald Trump na mpinzani wake wa chama cha Democratic walitumia siku nzima ya Jumatatu kuwashawishi wapiga kura kuwapatia ushindi.

Katika mkutano wa kampeni kwenye jimbo lenye ushindani mkali la North Carolina, rais Trump alimtaja hasimu wake Joe Biden "kama mwanasiasa wa siku nyingi asiyewapenda raia wa Marekani" huku yeye akijitambulisha kama "mgeni wa siasa atakayewalinda raia wa nchi hiyo kwa kiwango cha juu".

Trump ambaye amekuwa rais kwa miaka minne iliyopita hakuwahi hapo kabla kushika nafasi ya uongozi na anajaribu kujitofautisha na Biden, seneta na makamu wa rais wa zamani ambaye amekuwepo kaitka siasa za Marekani kwa miongo minne iliyopita.

Katika kampeni za lala salama, Biden alifanya mkutano kwenye jimbo tete la Ohio na kutumia hotuba yake kumshambulia Trump kama kiongozi dhaifu, asiyeweza kujitoa muhanga na asiyefahamu chochote kuhusu umuhimu wa kuwa jasiri.

Biden aliyeongozana na wajukuu zake wanne kwenye mkutano mjini Ohio amesema Trump amegeuka na kuwa kituko mbele ya viongozi wengine wa dunia.

Kila upande unajaribu kutafuta walau kura ya mwisho 

USA Miami | US-Wahl | Biden und Trump Anhänger
Picha: dpa/picture-alliance

Kwa kuwa hadi sasa hakuna anayetabiriwa kwa uhakika kuwa mshindi. Timu za kampeni za kila upande zinatumai mikutano ya mwisho mwisho inaweza kubadili mweleko wa wapiga kura.

Kampeni ya rais Trump imetuama kumpaka matope Biden kuwa atavuruga uchumi pindi atatangaza vizuizi vikali vya kukabiliana na janga la virusi vya corona pamoja na kupandisha kodi kwa matajiri.

Kadhalika anadai wanasiasa na wafuasi wa chama cha Democratic wanagemea siasa za Ujamaa kwa kuruhusu mipaka kuwa wazi na kupinga sekta ya uzalishaji nishati inayochafua mazingira.

Biden ambaye kwa tajriba yake ni mwanasiasa anayegemea sera za wastani za mrengo wa shoto ameahidi kulinda haki ya wamarekani kupata huduma za afya, mafao kwa wazee na kutengeneza nafasi mpya za kati kupitia sekta ya nishati jadidifu.

Kwenye hotuba zake za mwisho, Biden kwa sehemu kubwa amemkosoa rais Trump kwa jinsi alivyoshughulikia janga la virusi vya corona,akimtuhumu kupuuza kuchukua hatua stahiki na badala yake kusababisha vifo vya mamia kwa maelfu ya wamarekani.

Hadi kufikia sasa wamarekani milioni 97 kati ya milioni 225 wenye sifa ya kupiga kura tayari wameshiriki upigaji kura wa mapema na kuweka rekodi ya kuwa idadi kubwa kabisa ya watu kujitokeza kushiriki uchaguzi kabla ya kilele ambayo ni siku ya uchaguzi.

Kuna ishara za wazi kuwa matakeo ya uchaguzi wa leo yataishia mahakamani kufuatia timu ya kampeni ya Trump kusema watafungua kesi iwapo zoezi la kuhesabu kura litarefushwa kuruhusu kura zilizopigwa kwa njia ya posta kuwasili na kuhesabiwa.

Biden pia tayari ameandaa kikosi cha wanasheria kukabiliana na shauri lolote kutoka upande wa Trump.