Trump apelekwa hospitali baada ya kupata COVID-19
3 Oktoba 2020Rais wa Marekani Donald Trump Ijumaa amepelekwa katika hospitali ya kijeshi kupatiwa matibabu baada ya kukutikana na ugonjwa wa COVID-19.
Trump amehamishiwa katika hospitali ya Walter Reed saa 17 baada ya kugunduliwa kuwa na ugonjwa huo.
"Hali yangu inaendelea vizuri," Trump ameonekana akisema katika vidio fupi aliyoituma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.
Kellyanne Conway, meneja wa kampeni za Trump za 2016, amesema naye pia amepata ugonjwa wa COVID-19. "Dalili zangu ni za mbali (kikohozi kidogo) na ninajisikia vizuri. Nimeanza mchakato wa kujitenga kwa kushauriana na madaktari," Conway ameandika Twitter.
Msemaji wa Ikulu ya White House Kayleigh McEnany amesema Trump atafanya kazi katika chumba maalum hospitalini kwa siku chache zijazo kama hatua ya tahadhari.
Trump kupewa dawa bado inayofanyiwa majaribio
Inasemekana kwamba Trump mwenye umri wa miaka 74, anasumbuliwa na homa na kwamba atapewa dawa ambayo bado inafanyiwa majaribio.
Trump, ambaye amekuwa akikana kishio cha virusi vya corona tangu janga hilo lilipoanza, aliandika kwenye Twitter mapema Ijumaa kwamba yeye na mkewe Melania watalazimika kujitenga baada ya kupimwa na kukutwa na virusi hivyo, ambavyo vimeua zaidi ya Wamarekani 200,000 na kuharibu vibaya uchumi wa taifa hilo.
Trump yuko katika hatari kubwa kwa sababu ya umri na uzito wake wa mwili.
Ugonjwa wa COVID-19 umesimamisha kampeni za rais huyo ikiwa zimebakia siku 31 pekee hadi siku ya uchaguzi. Wasimamizi wa kampeni za Trump wamesema mikutano yote na hafla nyingine zilizokuwa zimepangwa zitaahirishwa au zitafanyika mtandaoni.
Rais huyo wa Marekani wa chama cha Republican amepata ugonjwa wa COVID-19 akiwa katikati ya kampeni kuelekea uchaguzi wa mwezi Novemba ambapo atachuana na mpinzani wake wa chama cha Democratic Joe Biden.
Vyanzo: (rtre,dpa,ap)