Maradhi ya Buhari yaiyumbisha Nigeria
7 Juni 2017hali inayoamsha wasiwasi miongoni mwa raia kuhusu maradhi yanayomsumbua ambayo hayajawekwa wazi na kuiacha nchi hiyo yenye umaarufu mkubwa Barani Afrika bila ya kuwa na mwelekeo imara.
Kutokuwepo kwa kiongozi wa nchi hiyo kwa muda mrefu kunazusha "ombwe" anasema Msimamizi wa kampuni ndogo ya teknolojia ya mawasiliano iliyoko katika mji wa Lagos, ya Sprawling Computer Village, Dapo Alaba Sobowale, ambako kunapatikana maduka madogo na wachuuzi wanaosimama mitaani wakiuza simu za mkononi na vifaa vingine vya kielektroniki.
"Watu wengi wanamtegemea yeye" amesema Sobowale. Ameongeza kuwa hajali kuhusu ni nani hasa anashikilia madaraka yake hivi sasa, bali kinachompa wasiwasi na mtu aliyeko hapo kama atafanya maamuzi sahihi".
Buhari mwenye miaka 74, alienda Uingereza kwa ajili ya likizo ya matibabu Mei 7, kutokana na maradhi ambayo hayakuwekwa wazi. Tayari aliwahi kuwa London kwa karibu wiki saba mwanzoni mwa mwaka huu kwa ajili ya kupata matibabu. Alionekana mdhaifu aliporudi nchini Nigeria, na kushindwa kuhudhria vikao vitatu vya baraza la mawaziri. Aliporejea alisema hakuwahi kuugua namna ile katika maisha yake.
Maafisa wa serikali na familia ya Buhari walitaka kuwahakikishia Wanaigeria walioeleza kuingiwa na wasiwasi kuhusiana na kutokuwepo kwa kiongozi huyo kupitia mitandao ya kijamii kama vile "hashtag" zilizovuma sana mitandaoni za #WhereIsBuhari na #MissingPresident.
Mnamo siku ya Jumanne, mkewe Rais Buhari, Aisha Buhari alisema mume wake anapata nafuu haraka sana baada ya kurejea Nigeria akitoka kumtembelea hospitalini anakotibiwa, Jijini London. "Anawashukuru Wanaigeria kwa sala zao kwa ajili ya afya yake na kumtakia kuimarika haraka katika kipindi hiki cha changamoto." alindika bi. Buhari katika ukurasa wake wa twitter.
Kutokuwepo kwa Buhari kwa muda mrefu mwaka huu kumeibua maswali kuhusiana na iwapo kiongozi huyo wa zamani wa jeshi anayetokea Kaskazini mwa Nigeria ataweza kumalizia awamu yake ya miaka minne inayokamilika mwaka 2019 na kuanzisha minong'ono kuhusu nani atakayekuja baada yake.
Buhari alichaguliwa mnamo mwaka 2015 baada ya kumuangusha aliyekuwa rais wakati huo Goodluck Jonathan anayetokea Kusini. Kwenye kampeni aliahidi kukabiliana na rushwa na kupambana na kundi la wapiganaji wa itikadi kali la Boko Haram waliopo eneo la Kaskazini Mashariki mwa taifa hilo.
Wachambuzi wanasema, serikali ya Buhari iliyofikisha miaka miwili tarehe 29 ya mwezi May, ina rekodi nzuri na mbaya ya kutekeleza ahadi zake.
Pamoja na kwamba jeshi limefanikisha kuwaondosha wapiganaji hao wa Boko Haram kutoka maeneo ambayo walidai kuyatangaza ukhalifa, kundi hilo la wapiganaji wa Kiislamu wenye itikadi kali bado linaendeleza mashambulizi ya kujitoa muhanga.
Hii si mara ya kwanza kwa Nigeria kukumbana na hali kama hii ya kuwa na rais anayeumwa na kutokuwepo nchini kwa muda mrefu. Mwaka 2010, Rais Umaru Yar'Adua alifariki baada ya kuwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu kwa miezi kadhaa.
Makamu wa Rais Osinbajo asifika kwa uongozi wake.
Makamu wa Rais Yemi Osinbajo, ambaye kwa sasa anakaimu urais wa nchi hiyo anasifiwa kwa kurejesha kasi serikalini kwa kupunguza wasiwasi kwenye masuala ya usalama, hali ya mambo katika jimbo linalozalisha mafuta la Niger Delta na kuahidi kukabiliana na kuyumba kwa uchumi kulikochangiwa na kuanguka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
Hata hivyo, kama Osinbajo anayetokea Lagos iliyoko Kusini mwa nchi hiyo angechukua madaraka na kugombea urais katika uchaguzi ujao mwaka 2019, hatua hiyo ingeweza kuchukuliwa kama kitisho kwa watu wa Kaskazini cha kuchangia madaraka na kunaweza kusababisha machafuko ya kisiasa, wanasema waangalizi.
Wakosoaji wanasema kutokuwepo kwa Buhari kunadhihirisha kwamba serikali yake haiwezi kulirejesha taifa hili lenye utajiri wa mafuta kwenye kiwango chake cha awali.
Katika eneo hilo ambako kunapatikana maduka madogo na wachuuzi wanaosimama mitaani wakiuza simu za mkononi na vifaa vingine vya kielektroniki, mmoja wa wamiliki wa duka la simu Williams Akah na baadhi ya wateja wamesema watu wengi mjini Lagos wanapambana na changamoto za kushuka kwa uchumi wa nchi hiyo, hususan inakuja suala la kupata kazi zenye staha katika jiji hilo kubwa.
Akah hajui hasa nini kinachomsumbua Buhari, lakini anasema anafuatilia kila kinachomtokea kiongozi huyo. "Nina wasiwasi kuhusu hali yake, ni chaguo la kwanza la wananchi".
Mwandishi: Lilian Mtono/AP
Mhariri:Iddi Ssessanga