Mapigano mapya yaibuka kati ya Israel na Palestina
12 Aprili 2022Kijana huyo wa kipalestina alimchoma kisu afisa mmoja wa Israel wakati wa operesheni ya ukaguzi katika mji wa Ashkelon, hali iliyosababisha polisi kumuua kwa kumpiga risasi.
Mshambuliaji huyo aliye na umri wa miaka 40 anasemekana kutokea mji wa Hebron ulioko Palestina kusini mwa Ukingo wa Magharibi. Afisa aliyechomwa kisu alipata majeraha madogo.
Israel bado inaendeleza siku ya nne ya operesheni ya kulinda doria karibu na mji wa Jenin baada ya mshambuliaji katika mji huo kuwapiga risasi na kuwauwa watu watatu katika baa moja mjini Tel Aviv wiki iliyopita.
Soma zaidi:Jeshi la Israel ladaiwa kutekeleza mauaji Ukingo wa Magharibi
Usiku wa kuamkia leo Waziri Mkuu Naftali Bennett aliitembelea baa hiyo iliyofunguliwa tena huku akionya kuwa Israel haitokubali maadui wao kusitisha maisha ya watu wake na kuapa kupambana nao bila kuchoka.
Wakaazi:Mapigano yalitanguliwa na mirindimo ya risasi
Huku hayo yakiarifiwa wakaazi wa Jenin wameliambia shirika la habari la AFP kwamba vurugu hizo mpya zimetokea baada ya ufayatulianaji wa risasi uliofanyika katika siku za hivi karibuni.
Nalo shirika la habari la Palestina Wafaa limeripoti mapigano hayo kuzuka kati ya vijana wadogo wa kipalestina na wanajeshi wa Israeli walipoanza kushambuliana baada ya wanajeshi wa Israel kutumia risasi za moto na mabomu ya kutoa machozi dhidi yao. Jeshi la Israel halijasema lolote kuhusu tukio hili.
Soma zaidi:Mzozo wa Israel waripuka katika mkutano wa kilele wa AU
Hali katika eneo hilo imekuwa tata baada ya mashambulizi manne yanayodaiwa kufanywa na wapalestina kusababisha vifo vya waisraeli kadhaa ndani ya wiki mbili.
Israel yahofia ghasia zaidi
Israel inahofia kutokea kwa ghasia zaidi wakati huu ambako waumini wa kiislamu wako katika mfungo wa Ramadhani ulioanza mwanzoni mwa mwezi Aprili, na kabla ya sikukuu ya wayahudi na pasaka kwa waumini wa kikristo.
Mwaka uliopita vurugu mjini Jerusalem zilisababisha mapigano ya siku 11 kati ya Isral na wanamgambo wa Hamas wanaousimamia Ukanda wa Gaza.
Aidha Wapalestina pamoja na makundi ya kutetea haki za binaadamu wanadai jeshi la Israel linatumia nguvu kupita kiasi na mara nyengine linawajeruhi na kuwauwa watu ambao hawana hatia.
Wajumbe wa kidiplomasia wa Umoja wa Ulaya kwa ajili ya Palestina wameishutumu Israel pia kutumia nguvu kupita kiasi kuwadhibiti vijana wa kipalestina.
Chanzo: Mashirika