1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Israel vyauwa Wapalestina watatu

10 Juni 2021

Vikosi maalum vya usalama vya Israel vimewauwa Wapalestina watatu siku ya Alkhamis (Juni 10) katika makabiliano ya kutupiana risasi kwenye Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel.

https://p.dw.com/p/3uhf6
Libanon | Libanesisches Militär an der Grenze zu Israel
Picha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Wanajeshi wa kikosi hicho maalum walikuwa wameingia kwenye mji wa Kipalestina wa Jenin kwa madai ya kuwatia nguvuni watu wanaoshukiwa kuhusika na mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya wanajeshi wa Israel, kwa mujibu wa chanzo kimoja katika jeshi la Israel. 

Katika operesheni hiyo, wanajeshi hao waliwauwa maafisa wawili wa usalama wa Palestina na mtu mwengine mmoja, ambaye kundi la Islamic Jihad lilidai ni mwanachama wake.

Hata hivyo, chanzo hicho cha kijeshi kinasema kuna uwezekano kuwa maafisa hao wa usalama wa Palestina waliuawa kimakosa.

Ni nadra sana kwa vyombo vya usalama vilivyo chini ya serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina kupambana na wenzao wa Israel katika Ukanda wa Magharibi, na mara nyingi sana huwasaidia Waisrael kufanya operesheni zao kwenye eneo hilo.

Naibu gavana wa mji wa Jenin, Kamal Abu El-Rub, alisema askari kanzu wa Israel walimuua mtu mmoja na kumjeruhi mwengine wakati watu hao wakiwa wamekaa kwenye gari nje ya makao makuu ya idara ya upelelezi ya jeshi la Palestina.

Maafisa wawili wa usalama waliamuwa kurejesha mashambulizi na kisha nao wakauliwa, kwa mujibu wa El-Rub wakati akizungumza na shirika la habari la Reuters akiwa kwenye hospitali ambako maiti za watu hao zilipelekwa.

Palestina yailaumu Israel

Israel Golan-Höhen Panzer-Manöver
Vikosi vya IsraelPicha: JALAA MAREY/AFP/Getty Images

Chanzo cha usalama cha jeshi la Israel kilisema kwamba baada ya kutupiana risasi kwa mara ya kwanza na wanamgambo, maafisa wa usalama walioitwa kutoka kituo cha karibu waliwarushia risasi Waisraeli. 

"Inaelekea maafisa waliowarushia risasi walikuwa askari kanzu," kilisema chanzo hicho. "Vikosi vyetu vilirejesha mashambulizi, vikidhani risasi kutoka maafisa usalama wa Kipalestina zilikuwa zinarushwa na magaidi waliokuwa wakiwatafuta."

Hakukuwa na taarifa rasmi ya serikali ya Israel juu ya mkasa huo uliotokea usiku wa kuamkia Alkhamis.

Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina huratibu masuala ya usalama na Israel kwenye Ukingo wa Magharibi licha ya kukwama kwa mazungumzo juu ya mgogoro huo wa Mashariki ya Kati kwa muda mrefu sasa.

Wakati wa mashambulizi ya anga dhidi ya Ukanda wa Gaza mwezi uliopita, machafuko yalishuhudiwa pia katika Ukingo wa Magharibi.

Nabil Abu Rudeineh, msemaji wa Rais Mahmoud Abbas, alisema tukio hilo lilikuwa uchokozi wa hatari, na kwamba serikali ya Palestina inaamini Israel inapaswa kubeba lawama zote.