Bunge la Israel kuipigia kura serikali mpya
8 Juni 2021Spika wa Bunge Yariv Levin, ambaye ni mshirika wa Netanyahu, amesema hayo JUmanne, siku moja baada ya kukiri kwamba muungano mpya wa serikali ya mseto tayari umeshaundwa na upinzani.
"Mbunge Yair Lapid alimuarifu Rais na mimi kwamba amefaulu kuunda serikali mbadala. Kwa mujibu wa kifungu cha 13B, kikao cha bunge cha kuidhinisha serikali kitafanyika ndani ya siku saba, hiyo inamaanisha ifikapo tarehe 14 Juni 2021," amesema Yariv Levin, spika wa bunge la Israel.
Soma zaidi: Netanyahu apambana kuzuwia kuundwa serikali ya mseto
Muungano huo mpya unajumuisha vyama vinane tofauti vya kisiasa. Unatajwa kuwa ni muungano dhaifu wenye wingi mchache katika bunge hilo la Israel, Knesset, lenye viti 120. Hata hivyo licha ya udhaifu wake umeweza kuhimili kampeni kubwa ya upinzani iliyofanywa na wafuasi wa Netanyahu ikiwa ni pamoja na vitisho vya mauaji na maandamno nje ya nyumba za wabunge wa muungano huo mpya.
Netanyahu amemshutumu mshirika wake wa zamani Naftali Bennett kwa kumsaliti na kushirikiana na vyama vya siasa za mrengo wa kushoto na chama kidogo cha Kiarabu ambacho pia alikitaka kimuunge mkono.
Lapid na Bennett kupokezana wadhifa wa waziri mkuu
Bennett, mwenye siasa kali za kizalendo, atatumikia wadhifa wa waziri mkuu kwa miaka miwili, na baadaye atapokelewa na Yair Lapid wa siasa za wastani.
Israel imefanya chaguzi nne katika kipindi cha chini ya miaka miwili, wa hivi karibuni ikiwa umefanyika mwezi Machi.
Na katika kila uchaguzi, wapiga kura waligawanyika sana juu ya uwamuzi iwapo Netanyahu anapaswa kubakia madarakani huku, akiwa anakabiliana na madai ya ufisadi, ambayo kwa sasa amefunguliwa kesi mahakamani.
Serikali ya dharura iliyoundwa mwaka jana ili kushughulikia janga la virusi vya corona ilitawaliwa na vurugu za kisiasa na kusambaratika mwezi Desemba. Netanyahu alijaribu na kushindwa kuunda serikali baada ya uchaguzi wa Machi, kabla ya mamlaka hayo kupewa Lapid.
Soma zaidi: Mahasimu wa Netanyahu wakubaliana kuunda serikali
Hayo yote yanatokea katika wakati ambapo kuna mvutano mkubwa kati ya waandamanji wa Kipalestina na polisi ya Israel mjini Jerusalem, ambao hivi karibuni ulizua wimbi la vurugu za kikabila katika miji ya Israel na kusababisha mashambulizi ya siku 11 eneo la Gaza.
Vyanzo: ap,afp