1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu apambana kuzuwia kuundwa serikali ya mseto

3 Juni 2021

Baada ya kushindwa kuunda serikali, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameanzisha mapambano kuhakikisha muungano wa mrengo ya kulia, kati na kushoto wa Mayahudi na Waarabu havifanikiwi kuunda serikali mpya.

https://p.dw.com/p/3uOQy
Israel Premierminister Netanyahu - Chanukka
Picha: Getty Images/AFP/J. Guez

Kupitia mtandao wa Twitter, mwanasiasa huyo mkongwe anayekabiliwa na uwezekano wa kufutwa kwenye ramani ya kisiasa aliyoitawala kwa zaidi ya muongo mmoja, alitowa wito kwa wajumbe wa bunge la Knesset wanaoelemea mrengo wa kulia kupinga kile anachosema ni "serikali hatari ya mrengo wa kushoto", makhsusi akilenga kushiriki kwa mara ya kwanza kwa Waarabu kwenye serikali ya mseto nchini Israel.

Kiongozi huyo wa siasa kali za mrengo wa kulia aliamuwa kuelekeza mashambulizi yake kupitia mitandao ya kijamii siku moja baada ya mwanasiasa wa mrengo wa kati, Yair Lapid, kutangaza kwamba amefanikiwa kuunda serikali ya mseto, ikiwa ni dakika 35 kabla ya muda wa mwisho uliokuwa umewekwa, saa sita usiku wa kuamkia leo.

Muungano wa kisiasa uliotangazwa jana unatowa fursa kwa vyama vidogo na vya kati kushiriki kwenye uundaji serikali, kikiwemo chama kinachowakilisha asilimia 21 ya Waarabu wanaoishi ndani ya Israel, United Arab List (UAL).

Kwenye ujumbe huo wa Twitter, ambaye aliwahi kutupiwa lawama kali za ubaguzi baada ya kuwataka wafuasi wake kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa sababu "Waarabu walikuwa wakijazana vituoni kama njiwa", ameelezea mafungamano ya muungano huo mpya na kiongozi wa AUL, Mansour Abbas. 

Israel Wahl | Naftali Bennett
Naftali Bennett, waziri mkuu mtarajiwa wa Israel.Picha: Yonatan Sindel/AFP

Netanyahu, anayefahamika kwa uwezo wake wa kutumia fitina za kisiasa, ametuma vidio ya Bennet akisema kwamba Abbas "aliwatembelea wauaji walioko jela" baada ya mashambulizi ya mwaka 1992, ambapo raia wa Kiarabu waliwauwa wanajeshi watatu wa Israel.

Waarabu kuingia serikalini Israel

Chini ya makubaliano hayo, bilionea aliyekuwa waziri wa ulinzi na mwanasiasa anayetambuliwa kuwa na chuki dhidi ya Wapalestina, Naftali Benetti mwenye umri wa miaka 49, atakuwa waziri mkuu, kwa kipindi cha miaka miwili ya kwanza, kisha atakabidhisha nafasi hiyo kwa Lapid, waziri wa zamani wa fedha na aliyekuwa mtangazaji wa televisheni, mwenye umri wa miaka 57. 

Kikao cha bunge cha kuidhinisha serikali hiyo kupitia wingi mchache wa kura, kinatazamiwa kufanyika ndani ya siku 10 tangu tangazo kutolewa, muda unaompa nafasi Netanyahu kujaribu bahati yake tena kugeuza hali ya mambo na hivyo kuendelea kuhudumu kwenye nafasi yake ya uwaziri mkuu.

Makubaliano ya usiku wa jana kuunda serikali yalihitimisha ngwe ya kwanza ya majadiliano ya miezi miwili tangu uchaguzi wa Machi 23, ambapo si chama cha Likud cha Netanyahu na washirika wala wapinzani wao waliopata wingi wa kutosha bungeni kuunda serikali. Huo ulikuwa uchaguzi wa nne nchini Israel ndani ya kipindi cha miaka miwili.