Mitandao ya kijamii yasaini mpango wa kuzuia ujumbe wa chuki
16 Mei 2019Juhudi za viongozi hao, Rais Macron na Waziri Mkuu Ardern zilipewa msukumo na mashambulizi ya kigaidi dhidi ya miskiti nchini New Zealand mwezi Machi, ambayo yalionyeshwa moja kwa moja katika mtandao wa Facebook. Mtuhumiwa wa mauaji hayo ambaye ni mfuasi wa itikadi za kuwatukuza wazungu, aliurusha mubashara uhalifu wake kwa dakika kumi na saba, kabla ya Facebook kuzinduka na kuuzima mkanda huo. Tangu wakati huo, Waziri mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern amekuwa akiyahimiza makampuni ya mitandao kuchukua hatua.
Makampuni saba makubwa ya mitandao ya kijamii, yakiwemo Facebook, Youtube na Google yaitikia wito huo kwa kutia saini mpango wa kuondoa kabisa ujumbe wenye maudhui ya kigaidi na itikadi kali zinazohamasisha matumizi ya nguvu, kwa ushirikiano na Ufaransa, New Zealand na serikali za mataifa kadhaa mengine.
Hatua ya kupigiwa mfano
Makampuni hayo ambayo yanashirikisha pia Amazon, twitter, Microsoft na Dailymotion, yamejitwisha jukumu la kuhakikisha kwamba ujumbe huo wa chuki unaondolewa mara moja mtandaoni na kuzuiliwa kabisa kurejeshwa. Waziri mkuu Ardern amesifu juhudi hizo ambazo amesema hazina mfano.
''Mitandao ya kijamii ilihusika kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa, kuchochea mauaji ya mjiniChistchurch. Hatua zinazochukuliwa leo sambamba na wito huu pia hazijawa na kifani.'' amesema Bi Ardern na kuongezakuwa ''Haijatokea mataifa na makampuni ya mtandao kujumuika pamoja baada ya tukio baya la mashambulizi, na kushirikiana kuweka teknolojia mpya ambayo itazifanya jamii zetu kuwa salama zaidi.''
Kipigo kimoja kwa wakiukaji
Kulingana na mpango uliosainiwa na makampuni hayo yanayomiliki mitandao ya kijamii, makampuni hayo yatatekeleza sera iliyoitwa ''kipigo kimoja'', ambapo mtumiaji yeyote atakayevunja masharti makali dhidi ya maudhui ya chuki, atafungiwa mara moja uwezo wa kurusha chochote moja kwa moja mtandaoni kwa kipindi ambacho hakikubainishwa urefu wake.
Yametenga fuko la pamoja la dola milioni 7.5 za kuboresha teknolojia ya kutambua picha na video katika juhudi za kugundua maudhui mabovu yaliyoondolewa na kurudishwa tena kwa njia nyingine.
Viongozi wa Canada, Uingereza, Indonesia, Ireland, Senegal, Jordan na Norway, na pia rais wa Kamisheni ya Ulaya Jean Claude Juncker walishiriki katika mkutano huo ulioitishwa na Rais wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa New Zealand. Marekani haikushiriki katika mkutano huo, lakini mwenyeji, Rais Macron amesema kimsingi inaunga mkono ''Wito wa Christchurch'', ingawa uhuru wa kutoa mawazo bila ukomo ni suala tete kwa Wamarekani.
dpae,afpe