Idadi ya waliofariki yafikia watu 50 New Zealand
17 Machi 2019Wakati hayo yakifanyika ushahidi ulijitokeza wa ujasiri wa kutukuka pamoja na machungu ya mateso katika mashambulio ya bunduki ambayo yalichukua maisha ya watu 50.
Kamishna wa polisi Mike Bush amesema maafisa hatimaye waliweza kuwapatia familia orodha ya wahanga, kitu kilichocheleweshwa kutokana na haja ya kazi ya tahadhari ya polisi pamoja na kiwango cha mkasa huo. Kwa muda wa karibu siku tatu timu za uchunguzi wa alama katika matukio ya uhalifu , wengi wakiwa wamekuja kutoka sehemu mbali mbali za New Zealand , wamekuwa wakifanyakazi katika maeneo kadhaa ya uhalifu, katika misikiti ya Al Noor na Linwood pamoja na nyumba katika eneo la Dunedin, mji wa kusini mashariki ambako mtu anayeshukiwa kuwa ndie aliyefanya mashambulizi ya bunduki , aliishi.
Miili ya wale waliopigwa risasi na mtu huyo mwenye imani ya kuwa jamii ya wazungu ndio bora zaidi iliendelea kubakia ndani ya msikiti ikisubiri uchunguzi wa kitaalamu na utambuzi wa wanafamilia ambao wamekuwa katika hali ya kufadhaika mno ambao wanataka haraka kuanza taratibu za mazishi.
Tayari , matrekta ya kuchimba yameanza kazi katika eneo la makaburi mjini humo kuondoa mchanga unaohitajika kwa ajili ya kuwazika wahanga waliofariki.
Mara utambulizi utakapokamilika majina yatatangazwa, Bush alisema. Lakini tayari , taarifa za wahanga kutoka katika mataifa ya Kiislamu zimeanza kuonekana.
Mtoto mdogo yuko mahututi
Maafisa wa New Zealand wamesema watu 34 wanaendelea kuwapo Hospitali, wakitibiwa majeraha ambayo daktari Greg Robertson alielezea kuwa ni kutoka hali mbaya, majeraha ambayo yana ugumu wa kutibika kutokana na risasi, hadi "majeraha madogo madogo".
Miongoni mwa wale ambao wanatapia maisha yao ni pamoja na mtoto wa miaka minne Alin Alsati.
Mtoto huyo ambaye yuko katika shule ya chekechea alikuwa anasali kandoni mwa baba yake Waseeim katika msikiti wa Al Noor wakati aliposhambuliwa kwa risasi karibu mara tatu. Alipelekwa katika hospitali ya watoto ya Starship mjini Auckland kwa helikopta, ikiwa ni hospitali ya juu nchini humo ya kituo cha mifupa. Baba yake , ambaye pia alipigwa risasi, alihamia hivi karibuni nchini New Zeland kutoka Jordan na alikuwa ameanzisha duka la kinyozi , katika kitongoji cha Richmond.
"Tafadhali niombeeni na mtoto wangu wa kike," alitoa rai hiyo katika ujumbe wa vidio katika ukurasa wa Facebook akiwa hospitali kabla ya kufanyiwa upasuaji kuondoa vipande vya risasi na mfupa katika eneo lake la kiuno.
Mjini Christchurch, New Zealand na duniani kwa jumla kumekuwa na mikesha, sala, kumbukumbu na ujumbe wa mshikamano.
"Tuko pamoja na ndugu zetu Waislamu," ni maneno katika bango kubwa jekundu miongoni mwa maua mengi yaliyowekwa katika sehemu moja katika kile wakaazi waliochosema kuwa ni "mji wa huzuni".
Katika "kanisa kuu la mbao" mjini Christchurch, lililojengwa baada ya tetemeko la ardhi la mwaka 2011 ambalo bado limeweka doa katika mji huo , Dean Lawrence Kimberley aliendesha misa katika kuonesha "mshikamano na jamii ya waislamu."
"Tumejifunza wakati wa tetemeko kwamba katika wakati wa majaribu ni vizuri kunyoosheana mikono. Muda ni muafaka wa kufanya hivyo tena," amewaambia waumini.
Wakaazi waomboleza
Mjini Auckland , wakaazi wa jamii zote waliokuwa wakititikwa na machozi walisimama wakishikana mikono nje ya msikiti wa Umar kutoa heshima zao.
Katika eneo la bahari ya Tasmin , Waaustralia waliopatwa na mshituko kwamba kitendo kama hicho katika taifa hilo ndugu kimefanywa na mmoja wao, waliapa kutoa msaada wowote ule wanaoweza.
Mjini Sydney , tawi la fedha , ishara ya New Zealand, iliwekwa katika sehemu ya jengo la maarufu duniani la Opera.
Siku ya Jumamosi Tarrant alifikishwa mahakamani mjini Christchurch kukabiliwa na kile kinachotarajiwa kuwa moja kati ya mashitaka kadhaa ya mauaji.
Akisindikizwa na polisi wenye silaha, mkufunzi huyo wa zamani wa viungo alionesha ishara ya "okay" iliyopinduliwa ikiwa ni ishara inayotumiwa na makundi ya imani za nguvu ya uzungu duniani kote.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: John Juma