1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama Uganda yasikiliza rufaa dhidi ya sheria ya ushoga

18 Desemba 2023

Mahakama ya kikatiba nchini Uganda imeanza hii leo kusikiliza pingamizi la kwanza kuhusu sheria kali dhidi ya wapenzi wa jinsia moja, ambayo ilizusha ukosoaji mkubwa kutoka kwa Umoja wa Mataifa na mataifa ya Magharibi.

https://p.dw.com/p/4aHwT
Afrika Kusini | Maandamano dhidi ya sheria ya ushoga Uganda
Mahakama Uganda inasikiliza rufaa ya wanaharakati dhidi ya sheria ya ushoga.Picha: Themba Hadebe/AP Photo/picture alliance

Mahakama ya kikatiba nchini Uganda imeanza hii leo kusikiliza pingamizi la kwanza kuhusu sheria kali dhidi ya wapenzi wa jinsia moja, ambayo ilizusha ukosoaji mkubwa kutoka kwa Umoja wa Mataifa na mataifa ya Magharibi. Hata hivyo haijafahamika ni lini uamuzi wa mwisho unatarajiwa kutolewa.

Soma pia: Urusi yapiga marufuku vuguvugu la LGBT kwa itikadi kali

Sheria hiyo ilipelekea maafisa wa serikali kuwekewa vikwazo vya viza na Marekani na Rais Joe Biden alitishia kupunguza misaada na uwekezaji kwa taifa hilo la Afrika Mashariki lililopitisha mwezi mei mojawapo ya sheria kali zaidi duniani dhidi ya ushoga.
      
Lakini serikali ya Rais Yoweri Museveni imekuwa ikipuuzilia mbali ukosoaji huo huku maafisa wakizishutumu nchi za Magharibi kwa kile walichosema ni kujaribu kuishinikiza Afrika kukubali ushoga. 

Soma pia: Wanaharakati Uganda wakosoa EU kutochukua hatua dhidi ya sheria ya LGBTQ

Wanaotaka sheria hiyo kubatilishwa ni pamoja na wanaharakati kadhaa wa haki za binadamu, maprofesa wawili wa sheria kutoka Chuo Kikuu cha Makerere mjini Kampala na wabunge wawili wa chama cha Museveni cha National Resistance Movement.