Maandamano yanafanyika sehemu mbali mbali Ulimwenguni
15 Machi 2019Wanafunzi walitoka madarasani katika taifa la Australia na New Zealand na kuingia katika mwa miji mikuu ya nchi hiyo wakiandamana huku wakiwa wamebeba mabango yanayotoa ujumbe wa kuwasuta viongozi na kuwaeleza iwapo hawatachukua hatua kama watu wazima basi wao watoto watachukua hatua.
Maandamano hayo pia yaliwavutia maelfu ya watu waliojiunga nayo wakisema iwapo hatua hazitochukuliwa kuzuia gesi chafu inayotoka viwandani basi kila mmoja ataathirika. Maandamano makubwa zaidi yalifanyika Ulaya na Marekani.
Mmoja wa wanafunzi mjini Sydney Callum Frith akiwa katika maandamano hayo aliliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kwamba kama wanafunzi na vijana wameamau kutumia njia hiyo kuonyesha uwezo walionao katika kufanya maamuzi ya busara.
Naye mwanafunzi wa umri wa miaka 14 kutoka New Zealand alisema serikali inahitajika kufanya mabadiliko na ndio maana wameandamana siku ya masomo ili kuipa ujumbe mzito kuhusu hali inayoendelea kuwa mbaya ya mazingira.
Baadhi ya viongozi Ulimwenguni wawaunga mkono wanafunzi.
Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda Arden aliunga mkono mgomo wa wanafunzi hao na vilevile kuahidi kutenga dola milioni 68 kwa ajili ya kupunguza gesi chafu inayotoka viwandani.
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron pia waliunga mkono maandamano hayo.
Waziri wa Elimu wa Australia, Dan Tehan aliyapinga maandamano hayo na kusema iwapo wanafunzi wanaona jambo hilo ni muhimu wangelifanya siku ambazo sio za masomo.
Wanasayansi wanasema uchomaji wa nishati ya makaa ya mawe unasababisha gesi chafu ambayo inachangia kuongezeka kwa viwango vya joto ulimwenguni, hivyo kuleta mafuriko, ukame na kuongezeka kwa viwango vya maji baharini.
Katika kongamano la kimataifa kuhusu mazingira lililofanyika mjini Paris, Ufaransa mwaka 2015 mataifa yaliweka ahadi ya kuchukua hatua za kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya makaa ya mawe ili kupunguza kiwango cha joto kwa nyuzijoto mbili.
Kulingana na jopo la wanasayansi wa Umoja wa Mataifa, hali ya joto inazidi kuongezeka kote ulimwenguni, huku ripoti ya mwaka 2017 ikionyesha kwamba gesi chafu ya Carbon Dioxide imezidi.
(APE/RTRE)