1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron akwaa kisiki uundwaji wa serikali mpya ya Ufaransa

27 Agosti 2024

Rais wa Ufaransa Emmanuel anakabiliwa na kibarua kigumu kuitisha mazungumzo mapya ya kuunda serikali, baada ya vyama vya mrengo wa kushoto kukataa kushiriki tena kufuatia kumkataa mgombea wao wa nafasi ya waziri mkuu.

https://p.dw.com/p/4jycH
Ufaransa | Rais Emmanuel Macron
Rais Emmanuel Macron anakabiliwa na kibarua kigumu kuunda serikali baada ya uchaguzi wa bunge ambao haukutoa mshindi wa wazi.Picha: Julien De Rosa/AFP/Getty Images

Muungano wa vyama vya mrengo wa kushoto wa New Popular Front, NFP, uliibuka kwenye uchaguzi huo ukiwa kundi kubwa zaidi, lakini ukikosa wingi wa kutosha kuweza kuunda serikali. Katika Bunge la Ufaransa lenye jumla ya viti 577, muungano wa NFP uma viti 190, ukifuatiwa na muungano wa Macron wa mrengo wa wastani wenye viti takribani 160 na chama  cha Marine Le Pen cha mrengo mkali wa kulia cha National Rally kilicho na viti 140.

NFP imemtaka Rais Macron kumteua mgombea wao Lucie Castets, mchumi mwenye umri wa miaka 37 mwenye historia ya harakati za mrengo wa kushoto. Lakini Jumatatu jioni, Macron aliondoa uwezekano wa kuteuwa serikali ya mrengo wa kushoto, akisema itakuwa tishio kwa utulivu wa kitaasisi. Badala yake, alitoa wito kwa viongozi wote wa kisiasa kuikabili hali hii ya mkwamo kwa kuonyesha moyo wa uwajibikaji.

Ofisi ya Macron ilisema haitakuwa na maana kuteua serikali ya NFP kwa sababu itakataliwa mara moja kupitia kura ya imani bungeni.

Rais huyo aliwatolea wito wasoshalisti, wanamazingira na wakomunisti katika muungano wa mrengo wa kushoto kushirikiana na mirengo mingine ya kisiasa, katika juhudi za dhahiri za kuvuta wanachama zaidi wenye msimamo wa wastani kutoka chama cha France Unbowed, LFI.

Macron akumbana na kisiki cha kambi ya kushoto

Lakini siku ya Jumanne kiongozi wa chama cha kisoshalisti Oliver Faure, alikataa miito ya Macron, na kusema hatakuwa mshiriki katika "demokrasia ya maigizo."

Soma pia:Matokeo ya uchaguzi wa bunge Ufaransa yatoa faraja Ulaya, baada ya wafaransa kuwanyima National Rally ushindi

Castets amemshtumu Macron kutaka kuwa rais, waziri mkuu na kiongozi wa chama kwa wakati mmoja, na kuongeza kuwa hii inawakosea heshima wapigakura wa Ufaransa na demokrasia.

Ufaransa | Rais Emmanuel Macron
Macron akiwa kwenye mahojiano mubashara, huku picha ya mgombea uwaziri mkuu wa muungano wa mrengo wa kushoto Lucie Castets, ikionekana kwenye skirini kubwa, Julai 23, 2024.Picha: Ludovic Marin/AFP/dpa/picture alliance

Mwanzilishi wa chama cha LFI, Jean-Luc Melenchon alikwenda mbali hata kutishia kuazisha mchakato wa kumuondoa Macron madarakani.

Wanachama wa kambi ya Rais wamesema kwamba Macron hakutarajia kambi ya kushoto kupinga juhudi zake za kuwagawa. "Macron aliipuuza sana kambi ya kushoto," alisema mshirika mmoja wa rais, akiomba asitajwe jina.

Mwanachama wa serikali ya muda aliongeza kuwa yumkini washauri wa Macron hawakuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu utendaji wa ndani wa muungano wa NFP. "Macron hana wanasiasa wengi wa mrengo wa kushoto upande wake. Wote wameondoka," alisema waziri huyo, pia akiomba kutotajwa jina.

Mrengo mkali wa kulia wamtupia lawama Macron kwa kuvuruga nchi

Chama cha mrengo mkali wa kulia cha National Rally, RN, hakijaalikwa kwenye mazungumzo ya Jumanne, yalioanza kwa Macron kukutana na kundi la wabunge wasio na vyama. Viongozi wa chama hicho cha RN wamemshtumu Macron kwa kusababisha hali hiyo ambayo Marine Le Pen ameifananisha na machafuko.

Soma pia:Jukumu la Macron katika Umoja wa Ulaya huenda likadhoofishwa na duru ya pili ya uchaguzi 

"Emmanuel Macron amechagua machafuko. Tunahisi anayafanya machafuko haya yadumu hadi mwezi Septemba, na hii ndiyo imekuwa hali kipindi chote cha kiangazi. Siwezi kukupa jibu, ni machafuko, siwezi kutoa suluhisho, ni machafuko. Ni machafuko tuliohofia yangekuja," alisema Le Pen.

Macron ashinda awamu ya pili ya urais

Siku ya Jumatano, atakutana na wawakilishi kutoka Les Republicains, chama cha mrengo wa kati wa kulia, na idadi kadhaa ya wanasiasa wa kihafidhina.

Wakati huo huo, Francois Bayrou, veterani anaeheshimika wa mrengo wa kati, alimkosoa rais kwa kupoteza muda katika majadiliano ya vyama, ambayo alisema yalikuwa "mbinu isiyo sahihi."

Badala yake, alisema, Macron anapaswa kutafuta mgombea mwenye uzoefu na ofisi ya juu. "Kuna watu walioshikilia ofisi ya rais," alisema, "wengine walioshika nyadhifa za juu serikalini," au "waliowakilisha mavuguvugu ya kisiasa na mawimbi."

Ofisi ya Macron haijatoa ishara yoyote kuhusu ratiba ya rais huyo kuteuwa waziri mkuu - lakini muda unayoyoma kuelekea Oktoba 1, ambayo ndiyo tarehe ya mwisho ambapo serikali inapaswa kuwa imewasilisha sheria ya bajeti kwa mwaka 2025. 

Marcon amepangia kufungua michezo ya olimpiki ya walemavu hapo kesho Jumatano, na anatarajiwa nchini Serbia siku ya Alhamisi kwa ziara rasmi.