1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC: Waasi wa M23 waishambulia kambi ya kijeshi ya Mubambiro

7 Machi 2023

Kundi la waasi wa M23 wameishambulia kambi ya kijeshi ya Mubambiro iliyopo nje kidogo na mji wa Goma na ambayo inawahifadhi wanajeshi wa Burundi waliowasili nchini humo siku chache zilizopita.

https://p.dw.com/p/4OL5M
Kongo I Treffen zwischen EACRF und  M23-Rebellen
Picha: Guerchom Ndebo/AFP

Mashambulizi hayo ya jana yalitokea wakati mapigano makali yalikuwa yakiendelea kati ya jeshi la Kongo na waasi hao kwenye vijiji vya Karuba na Malehe wilayani Masisi, ambako milio ya risasi ilisikika siku nzima ya jana Jumatatu.

Kulingana na taarifa ya jeshi la Kongo, waasi wa M23 walifyatua maroketi kuelekea kwenye mji wa Sake na kuwauwa watu  wawili na wengine kadhaa kujeruhiwa kabla ya kulengwa kwa kambi ya kijeshi Mubambiro mbali kidogo na mji wa Goma, alifahamisha Njike Kaiko, msemaji wa gavana kijeshi mkoani Kivu Kaskazini.

Soma pia: Wanajeshi wa Burundi wawasili DR Kongo

Akizungumza na DW, Telesphore Mitondeke ambaye ni mratibu wa shirika la raia wilayani Masisi, amelaani shambulio hilo la waasi hao waliolenga nyumba za wakaazi na kuongeza hofu mkubwa katika mji huo wa Sake ambao maelfu wameshaukimbia na kuelekea Goma.

Licha ya waasi hao wa M23 kutakiwa kuheshimu mkataba wa mwisho wa mkutano mdogo uliofanyika mjini Luanda nchini Angola uliowakata kurejea katika nafasi yao ya awali kwenye milima ya Sabinyo kuanzia leo Jumanne, lakini hadi mchana huu waasi hao wamevidhibiti vijiji vya Kibirizi, Kabanda na Kirima katika wilaya ya Rutshuru ambako maelfu wa raia wanahangaika ndani ya msitu.

Soma pia: Barabara muhimu zafunguliwa Kivu Kaskazini

Uasi wa kundi la M23 umesababisha kuchochea mzozo kati ya Kongo na Rwanda, ambapo kinshasa imekuwa ikiutuhumu utawala wa Kigali kuwasaidia waasi hao, shutuma zinazokanushwa vikali na Rwanda.