Mzozo wa Kongo wajadiliwa Bujumbura
4 Februari 2023Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wako nchini Burundi kwa mkutano wa kilele wa kikanda kujadili mgogoro wa mashariki mwa Kongo.
Mazungumzo hayo yanafanyika mji wa kiuchumi wa Burundi, Bujumbura na yameandaliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo inaongoza juhudi za upatanishi zikilenga kumaliza vita vinavyoendeshwa na makundi ya waasi Mashariki mwa Kongo.
Jumuiya ya Afrika Mashariki Ijumaa iliandika ujumbe kwenye mtandao wa Twitta ikifahamisha kwamba ajenda ya mkutano huo ni kutathmini hali ya usalama mashariki mwa Kongo na kutazama namna ya kuendelea mbele.
Rais Paul Kagame wa Rwanda anayetuhumiwa kuyaunga mkono makundi ya waasi mashariki mwa Kongo nae pia ni miongoni mwa viongozi wanaoshiriki mkutano wa Bujumbura.
Ni mara ya kwanza kwa Kagame kwenda Burundi tangu mwaka 2013 alipohudhuria sherehe za uhuru.
Nchi hizo mbili jirani za eneo la maziwa makuu kwa muda mrefu zilikuwa kwenye mahusiano ya mashaka kila mmoja akimtuhumu mwenzie kwamba anaingilia masuala yake ya ndani .
Mwaka 2020 Kagame alimtolea mwito rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye wakati huo akiwa ndo kwamba amechaguliwa kuingia madarakani,kuyabadilisha mahusiano ya kidiplomasia lakini mwito huo ulipingwa na Burundi iliyosema ni mwito wa kinafiki.Kenyatta atoa wito wa kupunguza mzozo DR Kongo
Burundi imekuwa ikiishutumu Rwanda kwa kuwapa hifadhi wale waliohusika kwenye mapinduzi yaliyoshindwa mwaka 2015 yaliyoitumbukizwa nchi hiyo katika machafuko.
Ofisi ya rais wa Burundi imetuma picha kwenye ukurasa wa Twitta ikimuonesha rais Kagame akiwasili pamoja na viongozi wengine wa nchi akiwemo rais wa Kenya William Ruto, rais wa Uganda Yoweri Museveni na Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.
Japokuwa ofisi ya rais wa Kongo Ijumaa ilifahamisha kwamba rais Felix Tshisekedi atakwenda Bujumbura kuhudhuria mkutano huo wa kilele,kufikia mchana bado alikuwa hajaonekana.