1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Lukashenko: Tunaiunga mkono China kuhusu Ukraine

1 Machi 2023

Rais wa Belarus Alexander Lukashenko amemwambia Xi Jinping wa China kwamba nchi yake inaunga mkono kikamilifu mapendekezo ya Beijing ya kuumaliza mzozo wa Ukraine kwa mazungumzo na suluhu ya amani.

https://p.dw.com/p/4O7fq
Peking Treffen Präsident Lukaschenko und Xi Jinping
Picha: PAVEL ORLOVSKY/BELTA/AFP

Rais wa Belarus Alexander Lukashenko amesema hayo alipokutana kwa mazungumzo na Xi mapema leo, huku mapigano makali yakiendelea kushuhudiwa katika mkoa wa Bakhmut nchini Ukraine, ambapo wanajeshi wa Ukraine wanapambana kuzuia jaribio la Urusi la kuukamata mji mdogo katika mkoa huo. 

Muasisi wa kundi la wanajeshi mamluki Wagner la nchini Urusi Yevgeny Prigozhin, amesema hii leo kwamba mapigano ni makali na kukiri wanajeshi wa Ukraine wanajaribu kuwazuia kwa kila hali kuudhibiti mji huo mdogo katika eneo la Bakhmut.

Wapiganaji wa Wagner wamekuwa wakiongoza mashambulizi katika eneo la mashariki mwa Ukraine kwa miezi kadhaa sasa, wakati Moscow ikiutizama mkoa huo kama kiungo muhimu kabisa kitakachowasaidia kuidhibiti miji mkubwa zaidi kama ya Kramatorsk na Sloviansk.

Katika siku za karibuni, makamanda wa Ukraine wamekuwa wakionya kwamba hali ni tete kwenye mkoa huo na inazidi kuwa mbaya kila uchwao, wakati Urusi ikizidi kuongeza mashambulizi kwa lengo la kuuzingira. Lakini maelfu ya raia wa ukraine na wanajeshi wanakabiliana vikali na wavamizi hao na wengine maelfu wanajifungia kwenye majumba yao yaliyoko kwenye mji huo uliowahi kukaliwa na karibu watu 70,000.

Kazakhstan USA
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken akipeana mkono na rais wa Kazakhstan Kassym-Jomart Tokayev, wakati akiwa ziarani nchini humo ili kuimarisha mahusiano.Picha: Olivier Douliery/picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Akiwa mjini Tashkent, akimalizia ziara yake kwenye eneo la Asia ya Kati waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Anthony Blinken amesisitiza ya kwamba ni rais Vladimir Putin tu mwenye nafasi kubwa ya kuhakikisha vita hivi viamalizika kwa kuwa ndiye aliyevianzisha na kuongeza kuwa anaamini watu ya Ukraine ndio wanaotaka amani zaidi ya mtu yoyote mwingine kwa kuwa wao ndio wahanga wakuu.

"Hakuna anayetaka amani haraka zaidi kuliko watu wa Ukraine. Wao ni wahanga wa kila siku wa uchokozi wa Urusi. Na kama amani ingepatikana hata hapo kabla, wangekubali. Na sisi pia tungeipokea, na hata mataifa yote ulimwenguni yanayoteseka, kutokana na athari za uchokozi wa Putin. Sote tunajua ukweli kwamba vita vinaweza kumalizika kesho au hata leo. Putin aliyeamua kuvianzisha, anaweza kuvimaliza. Na hatupaswi kamwe kuusahau ukweli huo."

Hapo jana Blinken alikutana na mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa yote matano ya ukanda huo huko Kazakhstan na hii leo amezuru Uzbekhistan na kukutana na rais Shavkat Mirziyoyev.

Rais Alexander Lukashenko naye akiwa ziarani Beijing, China ambaye ni mshirika kindakindaki wa rais Vladimir Putin amesema wanaunga mkono kikamilifu mapendekezo ya taifa hili kuhusu amani kwa njia ya mazungumzo. Ingawa wafuatiliaji wa mambo na mataifa ya magharibi wamekuwa na mashaka na msimamo huo wa China ambayo imekataa kulaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, lakini Lukashenko anasisitiza hii leo kwamba wako nyuma ya mapendekezo hayo.  

UN-Generalversammlung zum Ukraine-Konflikt in New York
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ajipanga kuzipangua propaganda zozote kuhusu Urusi kwenye mkutano wa G20, New Delhi. Picha: John Angelillo/UPI/IMAGO

Blinken aondoa uwezekano wa kukutana na mawaziri wa Urusi na China.

Katika hatua nyingine, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema anapanga kukabiliana na propaganda yoyote ya Urusi itakayoibuliwa katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la mataifa yaG20 huko New Delhi nchini India, hii ikiwa ni kuingana na msemaji wa wizara ya mambo ya nje nchini humo.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov anahudhuria mkutano huo n tayari amefanya mazungumzo na mwenzake wa India Subrahmanyam Jaishankar mapema leo, kabla ya kuanza kwa mkutano huo kesho Alhamisi.  Mawaziri hao wawili walijadiliana kuhusu hali ya usalama katika muktadha wa mzozo wa Urusi na Ukraine na mahusiano ya kibiashara baina yao.

Lavrov pia alikutana na mwenzake wa Uturuki na kufanya mazungumzo pia na waziri wa mambo ya nje wa China, Bangladesh na Afrika Kusini.

Ingawa mkutano huu unawakutanisha ana kwa ana mawaziri hawa wa mambo ya kigeni, lakini Blinken wa Marekani tayari ameondoa kabisa uwezekano wa kukutana na mawaziri wa Urusi na China, huku akiishutumu Moscow kwa kutokuwa na nia ya dhati ya kuvimaliza vita vyake nchini Ukraine na kuongeza kuwa atakutana nao katika vikao vya kawaida vitakavyofanyika kwenye mkutano huo.

Soma Zaidi: Mawaziri wa mambo ya nje wa G20 wakutana India