Libya yasitisha uzalishaji wa mafuta
27 Agosti 2024Makundi ya Libya yameingia kwenye mvutano wa kuwania madaraka juu ya udhibiti wa benki kuu na mapato ya mafuta ya nchi hiyo.
Duru ya hivi punde zinaarifu kuwa mvutano uliibuka baada ya juhudi za mirengo ya kisiasa kumwondoa madarakani mkuu wa Benki Kuu ya Libya (CBL) Sadiq al-Kabir, huku makundi hasimu yenye silaha yakikusanyika kila upande.
Soma pia: Libya yakabiliwa na kitisho cha kuporomoka kwa uchumi
Mapema siku ya Jumatatu, serikali yenye makao yake makuu mashariki mwa Libya ilitangaza kuwa maeneo ya mashariki ya mafuta, ambayo yanachangia karibu uzalishaji wote wa nchi, yatafungwa, na uzalishaji na uuzaji nje utasitishwa kufuatia mizozo inayoongezeka juu ya uongozi wa Benki Kuu ya Libya.
Shirika la habari la Reuters hii leo, limeripoti kuwa viwanda viwili vya mafuta kusini mashariki mwa Libya vimesimamisha uzalishaji huku kingine kikipunguza uzalishaji.
Wasiwasi miongoni mwa raia
Hii imesababisha mfadhaiko miongoni mwa mwa Walibya, ambao wanasema wanataka tu kuendelea na maisha yao ya kila siku kama kawaida. Kama anavyoeleza Salem Khalil.
"Tunadai taratibu zote za benki zirudi kama zilivyokuwa, kuhusu matatizo ya kisiasa na ushindani wa uongozi wa Benki Kuu wasuluhishe wenyewe na wananchi wawe na uwezo wa kufanya shughuli zao za kibenki kama kawaida. Kuhusu kufungwa kwa visima vya mafuta, hali hii itasababisha Libya kupoteza fedha."
"Tumekuwa tukishuhudia kufungwa visima vya mafuta mara kwa mara hapo awali, hatimaye vitafunguliwa lakini matukio haya, athari zake zitakwenda moja kwa moja kwa raia."
Hata hivyo hakukuwa na uthibitisho kutoka kwa serikali inayotambuliwa kimataifa huko Tripoli au kutoka kwa Shirika la Mafuta la Kitaifa, ambalo linasimamia rasilimali za mafuta za Libya. Wakati sehemu kubwa ya visima vya mafuta viko chini ya kamanda wa kijeshi Khalifa Haftar, kiongozi wa Jeshi la Kitaifa la Libya (LNA) mashariki mwa Libya.
Maamuzi ya upande mmoja
Huku haya yakijiri ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL umeeleze wasiwasi wake juu ya kile walichokitaja kama "hali inayozidi kuzorota ambayo imetokana na maamuzi ya upande mmoja.”
Migogoro kuhusu usimamizi wa benki kuu ya Libya imezua hofu kuhusu uwezekano wa matumizi mabaya ya raslimali za fedha nchini humo.
Aidha taarifa ya UNSMIL imeeleza kuwa, ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa nchini Libya umeitisha mkutano wa dharura na pande zote zinazohusika katika mgogoro juu ya usimamizi wa benki kuu ya Libya ili kufikia makubaliano yatakayozingatia maelewano ya kisiasa, sheria zinazotumika na kanuni ya uhuru wa benki kuu ya Libya.