Libya yakabiliwa na kitisho cha kuporomoka kwa uchumi
27 Agosti 2024Migogoro kuhusu usimamizi wa benki kuu ya Libya imezua hofu kuhusu uwezekano wa matumizi mabaya ya raslimali za kifedha nchini humo.
Taarifa ya UNSMIL imeeleza kuwa, ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa nchini Libya umeitisha mkutano wa dharura na pande zote zinazohusika katika mgogoro juu ya usimamizi wa benki kuu ya Libya ili kufikia makubaliano yatakayozingatia maelewano ya kisiasa, sheria zinazotumika na kanuni ya uhuru wa benki kuu.
Soma pia: Benki Kuu ya Libya yasitisha shughuli zake
Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa umetoa mwito wa kusitishwa kwa maamuzi ya upande mmoja, kuondolewa kwa hali ya dharura katika visima vya mafuta, kusitishwa kwa mivutano na hakikisho la ulinzi wa wafanyikazi wote wa benki kuu.
Uchumi wa Libya unategemea kwa kiasi kikubwa mapato yanayotokana na uuzaji wa mafuta.
Hata hivyo kumewekwa hali ya dharura katika visima vya mafuta, na hivyo kukatisha chanzo kikuu cha mapato ya nchi hiyo.
Mapema jana Jumatatu, utawala wa Libya upande wa mashariki uliamuru kufungwa kwa visima vya mafuta mashariki mwa nchi hiyo, hatua iliyositisha uzalishaji na usafirishaji wa mafuta baada ya kuibuka kwa mivutano kuhusu usimamizi wa benki kuu.