Kwa nini uchaguzi ni muhimu DR Kongo?
20 Desemba 2023Mamilioni ya watu wenye sifa za kupiga kura huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamepiga kura katika uchaguzi ambao unaoonekana kuwa kipimo kwa Rais aliye madarakani Felix Tshisekedi. Wapinzani wakuu wa Tshisekedi ni Moise Katumbi, Martin Fayulu, na Mshindi wa Tuzo ya Amani ya NobelDenis Mukwege.
Georges Bamue, Kijana wa miaka ishirini na saba ambaye pia ni dereva wa bodaboda anasema anasikitishwa mno na hali ya mambo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Miaka mitano baada ya kuhitimu diploma ya masuala ya kompyuta, mkaazi huyo wa Goma, mashariki mwa Kongo, bado anapitia wakati mgumu kupata kazi ama pesa za kuanzisha biashara kwa na fani aliyosomea.
Soma pia: Je, wagombea wanawake watabadili siasa za Kongo?
Akizungumza na shirika la habari la Reuters amesema na hapa namnukuu: "Nilijisemea mara tu baada ya kuhitimu, sasa angalau naweza kushuka kwenye baiskeli maana sasa hivi nimeipata diploma na sasa wanaweza kuniajiri lakini haikuwa hivyo." Mwisho wa kumnukuu.
Katika kazi anayofanya ya kuendesha bodaboda, Bamue anapata karibu dola 30, lakini kutokana na mfumuko wa bei uliokithiri wa Kongo, kushuka kwa thamani ya sarafu ya nchi hiyo, na mahitaji mengi ya kipato chake kidogo, anatatizika kujikimu kwa kulipa kodi ya nyumba na kuhakikisha familia yake inapata mahitaji muhimu.
Bamue, kama walivyo mamilioni ya Wakongomani wengine, ameshuhudia mabadiliko madogo tu ya hali yao ya kimaisha, licha ya utajiri iliyonao nchi hiyo tangu alipoingia madarakani Rais Felix Tshisekedi aliyeingia madarakani mwaka 2019.
Kongo Mashariki yamulikwa
Kuwepo kwa mapigano kati ya makundi hasimu yenye silaha mashariki mwa Kongo katika miaka ya hivi karibuni na uwepo wa vita vya kikanda vya miaka miaka mingi ambavyo vilipamba moto katika miaka ya 1990 na 2000 vinachochea kudhoofisha maisha ya raia wa nchi hiyo.
Soma pia:Kongo yachagua rais katikati mwa hofu ya udanganyifu
Kundi la M23 ambalo linadaiwa kuungwa mkono na Rwanda limeteka maeneo mengi tangu lianze kampeni zake mwaka 2021. Wapiga kura katika maeneo ya jimbo la Kivu Kaskazini linalokaliwa na wapiganaji wa M23 hawakuweza kupiga kura siku ya Jumatano.
Mbali na kundi hilo yapo pia makundi mengine kama vile ADF na CODECO, makundi yanayodai kuwa yanapigana mara kwa mara ili kutetea haki za wakulima.
Kwa upande mwingine Marekani imethibitisha utayari wake wa kufanya kila namna kuhakikisha kuwa inatumia nguvu yake ikiwemo kuwanyima visa wale wote ambao wataharibu mchakato wa uchaguzi nchini Congo.
Utajiri wa Kongo
Lakini moja ya sababu inayoufanya uchaguzi wa Kongo kuwa ni muhimu sana duniani ni kwamba Kongo ni mojawapo ya wazalishaji wakubwa wa maliasili ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wa dunia.
Kwa hivyo kuendelea kukosekana kwa utulivu na usalama mashariki mwa Kongo bila shaka kutaathiri uwezo wa makampuni ya kimataifa kupata rasilimali hizo ili kuziuza kwa usalama kwenye soko la kimataifa.
Soma pia:Upinzani Kongo wadai kuchezewa ´rafu` kuelekea uchaguzi
Hata hivyo, Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mtaifa linashughulika na wahamiaji ni kwamba zaidi ya watu milioni 26 nchini Congo wanahitaji msaada wa kiutu kufuatia athari za ukosefu wa usalama.
Watu wa Kongo wanasifika kwa ucheshi na ustadi wao katika kukabiliana na hali ngumu. Wengi wao hupenda kurejelea "Ibara ya 15" ya katiba, ambayo inalenga kuwaelekeza wananchi kutatua mambo yao wenyewe. Muziki pia una jukumu kubwa katika utamaduni wa nchi. UNESCO iliorodhesha mziki wa rumba wa Kongo kama urithi wa duniawa kitamaduni mnamo Desemba 2021.