Mamluki wa Urusi "Wagner" wazidi kujiimarisha barani Afrika
28 Oktoba 2024Kikosi cha mamluki wa Urusi, Wagner ambacho kwa miaka mingi kimefahamika kwa shughuli za kijeshi barani Afrika kinaendelea kupanua wigo wa shughuli na kujumuisha harakati za kiuchumi, kitamaduni na kijamii kwa lengo la kutetea maslahi ya Urusi barani Afrika.
Na tangu kiongozi wa Wagner Yevgeny Prigozhin, alipofariki katika ajali ya utata ya ndege baada ya kuingia katika mgogoro na Rais Vladimir Putin mnamo mwezi Juni mwaka 2023, kundi la Wagner limesogea karibu na serikali ya Urusi na kuwa wakala wa Urusi japo siyo rasmi.
Mtafiti wa mitaala ya kimataifa na kikanda kwenye chuo cha GIGA cha mjini Hamburg, Hager Ali, amesema "Kundi la Wagner ni muhimu kwa Urusi kwa sababu linaendeleza malengo rasmi ya kidiplomasia ya Urusi. Na kwa ajili hiyo serikali ya Urusi ndio mfadhili wa majeshi ya nchi kadhaa kushirikiana na nchi nyingine za jumuiya ya BRICS. Na kwa sababu sheria za kimataifa zinayahusu majeshi rasmi, kundi la Wagner linazingtiwa kuwa ni la wakandarasi tu.''
Baada ya kifo cha Prigozhin baadhi ya vikosi vya mamluki wa Wagner vimewekwa kwenye kitengo cha Afrika, lakini kikosi kipya kimewekwa chini ya usimamizi wa wizara ya ulinzi ya Urusi.
Wagner siyo mawakala pekee wa Urusi barani Afrika.
Urusi pia inafanya juhudi ya kueneza propaganda dhidi ya nchi za magharibi. Na ndiyo sababu Urusi imejenga taasisi za kitamaduni, ikiwa pamoja na ile ya mjini Bangui katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Mamia kadhaa ya watu wanajifunza lugha ya kirusi kwenye kituo hicho cha utamaduni.
Uhusiano kati ya mamluki wa Wagner na serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ni wa ndani sana. Mamluki hao wanamlinda rais wa nchi hiyo na pia wanashirikiana kwa ukaribu na majeshi ya nchi hiyo ili yaweze kutimiza lengo la kuidhibiti nchi hiyo inayokabiliwa na mgogoro.
Kwa mujibu wa taarifa, mamluki wa Kirusi kati ya 1,500 na 2,000 wapo katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Urusi na Jamhuri ya Afrika ya Kati zimetiliana saini mkataba juu ya ulinzi. Urusi inapanga kujenga kituo cha jeshi la anga. Chini ya mkataba huo kampuni za Urusi zinaendesha shughuli za mgodi wa dhahabu na uzalishaji mbao.
Soma pia:Mamluki wa Wagner wakiri wapiganaji wake wameuwawa pamoja na wanajeshi wa Mali
Na nchini Niger, mamluki wa Wagner wanaushikilia uwepo wa nchi hiyo kama anavyoeleza, Hager Ali mtafiti wa mitaala ya kimataifa na ya kikanda kwenye chuo cha GIGA cha mjini Hamburg.
Mamluki wa Wagner wanaweza kufanya shughuli mbalimbali barani Afrika pia kama kundi binafsi na hivyo kutowajibika juu ya sheria na mikataba ya kimataifa. Kwa sasa kundi hilo linashiriki katika mgogoro wa nchini Libya na pia kwenye eneo la Sahel.