Je, kifo cha Prigozhin kitamuimarisha Putin?
25 Agosti 2023Mwandishi wa habari za uchunguzi, Irina Borogan, ameiambia DW kwamba namna Yevgeny alivyouawa ndicho kitu kinachoendelea kuwaacha wengi wakiwa na maswali kwa kuwa tatizo ni kwamba ni vigumu kupata majibu ya mazingira ya kifo chake.
Mtaalamu wa masuala ya siasa kutoka nchini Austria, Gerhard Mangott, anaongezea kuwa "ni wachache wenye mashaka kwamba mkuu wa kundi maarufu la Wagner amekufa, na haiwezekani kwamba kifo hicho kilikuwa cha bahati mbaya na kuna uwezekano mkubwa kuwa mauaji hayo yaliamriwa na rais wa Urusi,Vladimir Putin."
Soma pia: Kremlin yakanusha kuhusika kifo cha Prigozhin
Anasema hatua hiyo huenda ikawa ni ya kulipiza kisasi baada ya Yevgeny kumuaibisha kufuatia jaribio lake la uasi mnamo mwezi Juni na kwa upande mwingine kama onyo kwa wakosoaji wanaomfuatafuata.
Mbali na Progozhin, ambaye duru za Urusi zinasema alikuwemo kwenye ndege binafsi iliyoanguka siku ya Jumatano, Dmitry Utkin, mwanzilishi mwenza wa kundi hilo binafsi la wapiganaji la Wagner pia inaaminika amekufa kwenye ajali hiyo.
Kuna ushahidi wa kujitosheleza kwamba ndege hiyo iliripuka ikiwa njiani kutoka Moscow kuelekea St. Petesburg.
Wengi walishangazwa na uasi wa Wagner dhidi ya Kremlin
Kwa muda mrefu, inaonekana kama kwamba mzozo kati ya Prigozhin na Putin ulisuluhishwa, lakini baada ya kamanda huyo kuongoza uasi dhidi ya uongozi wa kijeshi, Putin akamuita msaliti.
Hata hivyo, hakukuwa na lolote kubwa lililoonekana wazi kwa kuwa Prigozhin aliahidiwa kinga kutoka kwa waendesha mashitaka kwa kumtaka akaishi uhamishoni nchini Belarus.
Tukio hilo liliwashangaza Warusi. Kwamba katikati ya vita vyake nchini Ukraine, Prigozhin anapata ujasiri wa kuikabili Kremlin tena kijeshi!
Kwa masaa kadhaa, Putin alijikuta kama aliye dhaifu na asiye na nguvu yoyote.
Miezi kadhaa iliyopita, Prigozhin alitupiana maneno na mshirika wa karibu wa Putin na Waziri wa Ulinzi Sergei Shoigu pamoja na Mkuu wa Jeshi, Valery Gerasimov, akiwatuhumu kwamba jeshi limeshindwa kufanya majukumu yake.
Mahusiano ya Prigozhin na Putin yalianzia miaka ya 1990, na alikuwa mtu wa kwanza kuruhusiwa kuanzisha jeshi binafsi ili kusaidia misheni za Urusi nchini Ukraine, Mashariki ya Kati na Afrika.
Huko nyuma, Prigozhin alionekana kama mtiifu kwelikweli kwa Putin na kundi lake lilionekana kama lenye msaada mkubwa kwa Urusi katika kuiangusha Ukraine na hasa katika mashambulizi kwenye mji wa Bakhmut.
Athari kidogo huenda ikajitokeza katika vita vya Urusi nchini Ukraine
Wachambuzi wachache wanahisi kwamba tukio hili linaweza kuwa na athari katika vita vya Urusi nchini Ukraine, kwa kuzingatia kwamba kundi la Wagner, ambalo kwa sasa halina kiongozi, tayari lilikuwa limedhoofika katika mapigano makali yaliyoshuhudiwa katika majira ya machipuko.
Jeshi la Urusi nalo limekuwa katika mapigano makali bila ya msaada wa Wagnerkwa miezi mitatu iliyopita na lipo mahali pazuri kwa mtizamo wa Putin.
Swali hapa ni kwamba: nini kitatokea kwenye misheni za Wagner barani Afrika?
"Kundi hilo limefanya misheni nyingi chafu barani humo kwa ajili ya serikali ya Urusi na kwa kiasi kikubwa kuimarisha ushawishi wa Urusi kwenye mataifa kadhaa ya Afrika," anasema Mangott.
Soma pia: Yevgeny Prigozhin atangaza kuwasajili wapiganaji wapya
Anaongeza kile ambacho "hakikuwa dhahiri ni kwamba ni kwa muda gani Putin atakuwa amefanikiwa kuimarisha mamlaka yake".
Pengine hili linategemea namna atakavyofanikiwa katika vita vyake nchini Ukraine.
Kwa sasa, ni suala la muda tu kuona ikiwa Putin ataendelea kusimama pamoja na waziri wake wa ulinzi, kwani Prigozhin hakuwa mtu pekee aliyetaka Shoigu kubadilishwa.
Hata baadhi ya wazalendo na wanablogu wanaotambulika kitaifa kwa kuvipigia debe vita vya Urusi nchini Ukraine na ambao baadhi yao wamekutana na Putin ana kwa ana wametoa mwito kama huo wa Prigozhin.