Yevgeny Prigozhin atangaza kuwasajili wapiganaji wapya
22 Agosti 2023Hilo ni tangazo la kwanza la Prigozhin tangu alipoongoza uasi uliodumu kwa mfupi dhidi ya serikali ya Urusi mnamo mwezi Juni.
Mkanda wa video uliosambazwa kupitia kurasa za mtandao wa Telegram zenye mafungamano na kundi la Wagner, umemuonesha Prigozhin akisema kundi hilo linaendelea na operesheni zake za kuisaidia "Urusi kuwa dola yenye nguvu zaidi na kuyakomboa mataifa ya Afrika.
Amesema hivi sasa wanawasajili wapiganaji wenye uwezo mkubwa na wanaendelea kutekeleza majukumu ya kuundwa kwa kundi hilo.
Prigozhin alifahamika na wengi duniani mnamo mwezi Juni pale alipoongoza wapiganaji wake kufanya uasi dhidi ya mamlaka za Urusi unaotajwa kuwa ndiyo changamoto kubwa zaidi ya utawala wa miaka 23 wa rais Vladimir Putin.
Uasi huo ulipozimwa Prigozhin na wapiganaji wake walikimbilia nchini Belarus chini ya mkataba uliofikiwa kwa juhudi za rais Alexander Lukashenko wa nchi hiyo.