Kongo yakifungia kituo cha habari cha Al Jazeera
10 Januari 2025Kulingana na msemaji wa serikali ya Kongo, Patrick Muyaya, mamlaka ya nchi hiyo ilibatilisha kibali cha waandishi wa shirika hilo nchini humo na kwamba kituo cha Al Jazeera kilimuhoji mkuu wa mtandao wa ugaidi bila kuwa na kibali.
Siku ya Jumatano kituo cha televisheni cha Al Jazeera kilimuhoji Bertrand Bisimwa, Mkuu wa kundi la waasi la M23 linalopambana na jeshi mashariki mwa nchi.
Katika mahojiano hayo Bisimwa, aliishutumu serikali ya Kinshasa kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano mnamo mwezi Agosti na kudai kwamba kundi la M23 linaendesha "vita kamili vinavyoendelea."
Muyaya aliyafananisha mahojiano hayo kuwa sawa na kuukumbatia ugaidi na kwamba hilo halikubaliki na kuwataka wanahabari kutotoa fursa kwa magaidi.
"Niliamua, baada ya tathmini na mashauriano na timu yangu, kuondoa vibali vilivyotolewa kwa waandishi wa habari wa AlJazeera" Muyaya aliwaambia waandishi wa habari.
Soma pia:Waasi wa M23 wajaribu kuushambulia mji wa Sake
Aliongeza kwamba mara zote waandishi wa habari wameidhinishwa nchini DRC kufanya shughuli zao lakini kwa awamu hii kituo hicho amekishutumu kwa kutumia mtafiti ambaye anaiunga mkono Rwanda hadharani.
"wanawezaje kutumia mtafiti, ambaye ni mwanaharakati anayejulikana anayeunga mkono Rwanda ambaye hayumo kwenye orodha ya waandishi wa habari walioidhinishwa ambao watamhoji kiongozi wa vuguvugu la kigaidi bila ya kuwa na kibali au viza. Je, hiyo si dharau? "
Saa chache kabla ya kauli ya msemaji wa serikali ya Kongo, Waziri wa sheria Constant Mutamba kupitia mtandao wa X aliandika kwamba "mtu yeyote anayeripoti kuhusu shughuli za jeshi la Rwanda na wasaidizi wake M23 watakabiliwa na mkono wa sheria akimaanisha adhabu ya kifo.
Hata hivyo andiko hilo halikupewa msisitizo na msemaji wa serikali na badala yake alisema kauli ya waziri ililenga mtu anayeweza "kumtumikia adui".
Upinzani wakosoa matamshi ya serikali
Hata hivyo, upinzani nchini humo umekosoa serikali ya Kongo kukifungia kituo hicho na matamshi ya kutishia wanahabari.
Kupitia mtandao wa X msemaji wa upinzani, Hervé Diakiese, alisema uhuru wa kujieleza unamaanisha uwezo "sio tu wa kueneza propaganda za serikali bali pia mambo yanayoweza kuchukiza na kusababisha madhara.
Itakumbukwa kwamba siku ya Jumanne, bodi ya udhibiti wa vyombo vya habari nchini Kongo ilitoa onyo kwa vyombo vya habari vitatu vya nchini Ufaransa ikiwemo Radio France Internationale, France24 na TV5 Monde, kutokana na uandishi wao kuhusu harakati za waasi wa M23 mashariki mwa nchi.
Soma pia:Marekani yailaani M23 kwa kuvunja usitishaji mapigano
Baadhi ya wanaharakati nchini humo wamekosoa uamuzi huo wa serikali ya Kongo kwa kusema kulenga vyombo vya habari ni makosa. Jacques Issongo anasema
"Tunahitaji kujua hali ya usalama katika nchi yetu. Hatuwezi kuishi katika nchi ambayo hatuwezi kuwa na upande mwingine wa hadithi. Hatuko katika kanisa ambalo mchungaji au padri anasema na waumini wanasema: Amina. Ni muhimu tuwe na taarifa."
Hadi wakati huu kituo cha televisheni cha Al Jazeera hakijatoa tamko lolote kufuatia uamuzi huo wa serikali ya Kongo.