1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaJamhuri ya Kongo

Kongo: Kipenga cha kampeni za uchaguzi chapulizwa

Jean Noël Ba-Mweze
20 Novemba 2023

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Disemba 20 zimeanza kuanzia jana Jumapili. Rais Tshisekedi anayewania muhula wa pili alianza kampeni katika mji wa Kinshasa.

https://p.dw.com/p/4ZANd
 Rais Felix Tshisekedi na mgombea wa nafasi ya urais Jamhuri ya Kidemorkasia ya Kongo akiwa na wafuasi wake katika mkutano wa kisiasa
Rais Felix Tshisekedi na mgombea wa nafasi ya urais Jamhuri ya Kidemorkasia ya Kongo akiwa na wafuasi wake katika mkutano wa kisiasaPicha: JUSTIN MAKANGARA/REUTERS

Kampeini za uchaguzi nchini Kongo zinaendelea hii leo ambapo mgombea mkuu wa Upinzani Moise Katumbi anatarajiwa kuanzisha kampeini yake katika mji wa Kisiangani,mkoani Tshopo leo, kuwashawishi wapiga kura.

Rais anayetetea nafasi yake Felix Tshisekedi ni miongoni mwa waliozindua rasmi kampeini zao    hapo jana Jumapili.

Katika Uwanja wa mashujaa mjini Kinshasa  rais Félix Tshisekedi anayegombea tena urais kwa muhula wa pili, alianzisha kampeni yake ya uchaguzi.

Alisifu mafanikio yake akisisitiza elimu bila malipo na kueleza kwamba washirika wake wa zamani wa FCC, yaani muungano wa kisiasa wa raïs wa zamani Joseph Kabila walikuwa wakitilia mashaka.

Soma pia:Kampeni za uchaguzi mkuu kuanza rasmi tarehe 20.11.2023 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

"Nilipoanzisha elimu bila malipo, ndugu zetu wa FCC waliniambia kuwa sitafanikiwa," aliwaambia wapiga kura rais Tshisekedi.

Aliongeza kuwa kutokana na mshikamano ambao unashuhudiwa nchini humo aliona mwangaza wa kufanikiwa kwa sera hiyo ambayo ilikuwa ikipigwa vita na baadhi ya wanasiasa ikiwemo wapinzani.

Alisisitiza umuhimu wa kujitosa katika sera hiyo kwa kurumia rasilimali chache zilizopo.

 "Ni lazima kuanza na baadae ndipo tutajua kama tutafanikiwa au la.”

Washirika wa Tshisekedi wampigia debe

Baada ya kukomesha ushirikiano na FCC, Félix Tshisekedi aliunda muungano mpya uitwao Union sacrée de la nation.

Miongoni mwa maelfu ya wanaharakati wa muungano huo waliohudhuria mkutano wa jana ni Esther Mampuya.

Mkutano wa kisiasa wa rais na mgombea wa Urais Kongo Felix Tshisekedi
Wafuasi wa rais na mgombea Urais Kongo Felix Tshisekedi Picha: Justin Makangara/REUTERS

Anaamini kwamba kwa muhula wa pili, Félix Tshisekedi ataweza kuboresha na kuleta mageuzi katika sekta kadhaa.

"Tunachotaka ni kuweza kupata muhula wa pili ili kuonyesha uwezo aalionao katika kuleta mageuzi."

Mwanasiasa huyo aliongeza kwamba safu ya uongozi chini ya rais Tshisekedi imekuwa imara katika kukabiliana na mambo kadhaa ili kufanikisha dhima ya maendeleo ya taifa hilo ambalo linakabiliwa na kutetereka kwa hali ya usalama katika eneo la mashariki mwa nchi.

Soma pia:Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inatarajia kufanya uchaguzi Disemba 20, huku kukiwa na wasiwasi wa kiusalama

"Ana uwezo wa kubadilisha kile ambacho wengi wanadhani hakiwezekani, ataonyesha kile anachoweza katika muhula wake wa pili."  Alisema Esther.

Ponyo ajiondoa kwenye kinyang'anyiro

Upande wao, Martin Fayulu na Delly Sessanga ambao pia ni wagombea kiti cha urais nao walianzisha jana kampeni zao katika mikoa ya Kwilu na Kwango.

Augustin Matata Ponyo akijiondoa kwenye kinyang'anyirocha urais na kumuunga mkono mgombea Moïse Katumbi ambaye ni mmoja wa wapinzani wakuu wa Tshisekedi.

Kampeni sasa tayari zimeanzishwa kwa wagombea wa urais pamoja na wale wa ubunge wa kitaifa na wa mikoa.

Soma pia:Upinzani Kongo waazimia kuungana kuelekea uchaguzi Desemba

Desemba 4 ni zamu ya wagombea ushauri wa manispaa kuanzishwa kameni zao.

Vyama vya siasa vya upinzani Afrika vimetekeleza wajibu wao?