1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani DRC waazimia kuungana kuelekea uchaguzi Desemba

18 Novemba 2023

Wawakilishi kutoka vyama vinne kati ya vitano vikuu vya upinzani Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo walifanya mazungumzo nchini Afrika Kusini wiki hii kwa ajili ya kuunda muungano kuelekea uchaguzi wa mwezi ujao.

https://p.dw.com/p/4Z8JV
Moise Katumbi
Mmoja wa viongozi wa vyama vya upinzani Kongo, Moise KatumbiPicha: Nicolas Maeterlinck/BELGA/dpa/picture alliance

Mkutano huo wa Afrika Kusini uliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Transformation Initiative ITI na wakfu wa Koffi Annan. Msemaji wa mmoja wa wagombea wa urais Moise Katumbi, Olivier Kamitatu, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa majadiliano yalikuwa yenye tija na kilichosalia sasa ni kwa wagombea wenyewe kuuendeleza mchakato huo kwa lengo la kuwa na tiketi ya pamoja ya kuwania urais.

Soma zaidi: Wapinzani DRC wafanya mazungumzo Afrika Kusini

Kulingana na waandaaji wa mkutano huo, chama cha pekee ambacho hakikushiriki ni chama cha Edice, chake Martin Fayulu ambaye anadai kwamba yeye ndiye mshindi wa kweli wa uchaguzi wa mwaka 2018. Rais Felix Tshisekedi ndiye aliyetangazwa mshindi wa uchaguzi huo.