1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kipi atakachokumbukwa nacho Mwai Kibaki?

22 Aprili 2022

Rais wa 3 wa Kenya Mwai Kibaki aliyefariki dunia akiwa na miaka 90 aliliongoza nchi hiyo kwa miaka10, akishuhudia miaka iliyojaa umwagaji damu na rushwa na pia miaka ambayo Kenya ilijivunia kujipatia katiba yake mpya

https://p.dw.com/p/4AJCY
Ehemaliger Präsident Kenias Mwai Kibaki 2013
Picha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Kibaki aliyeingia madarakani mwishoni mwa mwaka 2002 na kuhudumu hadi 2013, alikuwa kiongozi shupavu na mahiri aliyejihusisha kwa muda mrefu na siasa za Kenya, kuanzia taifa hilo la Afrika Mashariki lilipojipatia uhuru wake mwaka 1963. 

Akitangaza kifo cha Mwai Kibaki mchana wa leo, rais wa sasa, Uhuru Kenyatta, alimtaja kama mwanasiasa muungwana na mwenye bashasha.

Lakini kama kiongozi aliyeingia madarakani mwaka 2002 kwa sera ya kupambana na ufisadi, uongozi wake ulikumbwa na visa vikubwa vya tabia hiyo, ambako mamilioni ya dola yaliibwa kutoka ofisi za umma nchini Kenya. 

Alipochukua madaraka kutoka kwa utawala wa kimabavu wa Marehemu Daniel Toroitich Arap Moi, Kibaki alikaribishwa kwa matumaini makubwa na Wakenya kuingoza nchi kutokana na ahadi zake za uwepo wa mabadiliko na ukuaji wa uchumi.  Mambo lakini hayakuenda kama alivyopanga.

Mkuu wa kwanza wa mamlaka ya kupambana na ufisadi nchini Kenya, John Githongo, aliwahi kusema kwamba Kibaki alionesha nia ya kupambana na ufisadi ila baadaye ikafahamika kuwa tabia hiyo imeshambaa sana na hivyo kulemaza juhudi za rais. Githongo aliyasema hayo katika kitabu cha muandishi wa Uingereza, Michela Wrong, kwa jina "Ni muda wetu sasa wa kula" akimaanisha muda wa kuendeleza na kufaidika na ufisadi.

Sakata kubwa zaidi likihusisha kesi ya mamilioni ya dola ya Anglo Leasing iliyoibuka mwaka 2004 ambako mamilioni ya fedha za umma yalilipwa kwa kampuni za kigeni kwa huduma tofauti ambazo hazikuwahi kutekelezwa.

Mazuri yaliyoonekana katika uongozi wake

Ehemaliger Präsident Kenias Mwai Kibaki 2012
Rais wa zamani wa Kenya hayati Mwai Kibaki Picha: Noor Khamis/REUTERS

Kando na hayo, uongozi wa Kibaki pia ulishuhudia mengi mazuri, kwa mfano, kupiga jeki sekta za afya na elimu zilizokuwa katika hali mbaya wakati wa tawala zilizopita. 

Alianzisha miradi mikubwa ikiwemo ile ya miundombinu na serikali yake pia ndio iliyokuwa ya kwanza kuanzisha elimu bure kwa watoto. Ushirikiano mzuri na China pia ulianzia chini ya utawala wake, hali iliyoinua uchumi wa nchi licha ya wachambuzi kusema kwamba kiu yake ya kutaka mabadiliko makubwa, ndio yaliyoiweka Kenya kuwa nchi iliyokopa kwa wingi.

Kingine kilichotokea katika uongozi wake ni kushuhudiwa kwa umwagikaji mkubwa wa damu mwaka 2007/2008 katika uchaguzi uliokumbwa na ghasia wakati watu zaidi ya 1,000 walipouwawa katika mapigano ya kikabila.

Kando na hayo kingine kikubwa ni pale Kenya ilipojipatia katiba mpya chini ya uongozi wake, ambao  Kibaki alijivunia nalo sana.

soma zaidi: Rais wa zamani wa Kenya Mwai Kibaki afariki dunia

Tangu kuondoka madarakani miaka tisa iliyopita, Kibaki aliyempoteza mke wake, Lucy, mwaka 2016, hakuwahi kuonekana sana hadharani.

Hali yake ya afya haikuwahi kuwa nzuri ikichangiwa na ajali ya barabarani mwaka 2002, siku chache kabla ya uchaguzi uliomuweka madarakani. Baada ya kustaafu, mara kwa mara alikuwa hospitalini kujiuguza.

Chanzo: afp