Rais wa zamani wa Kenya Mwai Kibaki afariki dunia
22 Aprili 2022Rais wa zamani wa Kenya Mwai Kibaki amefariki dunia. Kibaki aliyeitawala Kenya akiwa rais wa tatu wa nchi hiyo kuanzia mwaka 2003 hadi 2013 amefariki akiwa na umri wa miaka 90. Kifo chake kimetangazwa leo na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alimsifia Hayati kibaki na kumuita kama mtu aliyeongoza vyema.
Amesema ataendelea kukumbukwa kama mtu shupavu na mzuri katika siasa za Kenya aliyeliongoza taifa hilo katika maendeleo makubwa.
Kuteuliwa kwake kwa muhula wa pili mwaka 2007 kulitia doa uongozi wake baada ya mpinzani wake Raila Odinga kupinga matokeo ya uchaguzi.
Mwai Kibaki alisifika kwa kufufua uchumi wa Kenya uliokuwa umeporomoka ingawa kipindi cha uongozi wake kiligubikwa na vurugu mbaya zilizosababisha umwagikaji mkubwa wa damu kufuatia mvutano ulioibuka mnamo mwezi Desemba mwaka huo wa 2007 baada ya uchaguzi uliomrudisha tena madarakani. Aliiongoza Kenya kuanzia mwaka 2002 hadi 2013.
Rais Uhuru Kenyatta ametoa agizo la kufanyika maombelezo ya kitaifa ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti.
Chanzo: afp