1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa chama cha ANC Jacob Zuma mashakani

Charo, Josephat12 Machi 2008

Zuma aomba apewe muda kuchunguza ushahidi dhidi yake

https://p.dw.com/p/DNXT
Kiongozi wa chama tawala cha ANC nchini Afrika Kusini bwana Jacob ZumaPicha: AP

Mawakili ya serikali ya Afrika Kusini leo wameitaka mahakama kuu ya nchi hiyo kutupilia mbali jaribio la kiongozi wa chama tawala cha ANC, bwana Jacob Zuma, kuzuia ushahidi unaoonekana kuwa muhimu katika kesi inayomkabili. Wakati huo huo, kiwango cha biashara nchini Afrika Kusini kimeshuka kufikia kiwango cha chini kabisa kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka saba.

Wakili wa serikali ya Afrika Kusini, Wim Trengove, amemshutumu bwana Jacob Zuma mahakamani hii leo kwa kujaribu kuichelewesha kesi dhidi yake kupitia juhudi yake ya kuzuia matumizi ya stakabadhi zilizokamatwa kuhusiana na kesi ya rushwa inayomkabili. Trengove amewaambia majaji 11 wa mahakama ya katiba kwamba ikiwa serikali inataka kudhihirisha uaminifu basi hakuna haja ya kuuweka kando ushahidi uliopatikana dhidi ya bwana Zuma.

Kesi ya bwana Zuma ambayo imepangwa kuanza mwezi Agosti mwaka huu, huenda ikayaharibu matumaini yake kumrithi rais Thabo Mbeki ifikapo mwaka wa 2009. Kiongozi huyo wa chama wa African National Congress, ANC, anashtakiwa kwa kupokea rushwa ya kiwango cha mamia ya maelfu ya dola katika mkataba wa silaha.

Jana bwana Zuma aliwasilisha ombi katika mahakama ya katiba kutaka kesi iahirishwe ili alalamike dhidi ya misako ya waongoza mashtaka na kukamatwa kwa stakabadhi mnamo mwaka wa 2005.

Stakabadhi 93,000 zilikamatwa na kitengo cha uchunguzi cha Scorpions wakati wa uvamizi wa mwaka wa 2005 dhidi ya mali za bwana Zuma, wakili wake Michael Hulley na kampuni ya Thint, kitengo cha kampuni ya silaha ya kifaransa nchini Afrika Kusini, Thales. Kampuni hiyo itashitakiwa pamoja na bwana Zuma.

Washtakiwa wanataka wapewe muda kuchunguza uhalali wa stakabadhi hizo. Haijabainika wazi ni lini mahakama itakapopitisha uamuzi wake kuhusu ombi hilo.

Wakili Wim Trengove, akiiwakilisha serikali amesema hatua ya bwana Zuma kuomba apewe muda inachelewesha utekelezaji wa haki lakini akakasisitiza kiongozi huyo ana haki ya kuwasilisha ombi lake katika mahakama itakayosilikilia kesi yake. Trengove amesema serikali inaamini Jacob Zuma anaweza kupatikana na makosa katika kesi hiyo.

Iwapo bwana Zuma atapewa haki ya kulalamika, itazusha swali kubwa ikiwa vita vyake na vyombo vya sheria vitaendelea kwa mwendo wa kinyonga hadi kufikia kipindi cha uchaguzi wa rais.

Hii leo wakili wa bwana Zuma, Kemp J Kemp, amehoji kwamba haki ya kiongozi huyo wa chama cha ANC ya kutoingiliwa imekiukwa na kwamba waranti zilizotolewa kuruhusu uchunguzi wa kutia uchungu ufanywe dhidi ya bwana Zuma zilivuka mpaka.

Biashara imeshuka

Hatua ya bwana Zuma kupanda ngazi kisiasa imewatia wasiwasi baadhi ya wawekezaji, ambao wanahofu Afrika Kusini chini ya utawala wa kiongozi huyo huenda ikaondokana na sera za rais Thabo Mbeki zinazopendelea zaidi biashara.

Kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi iliyotolewa leo, uhakika wa kibiashara nchini Afrika Kusini kwa kipindi cha kwanza cha miezi mitatu ya mwaka huu, umeshuka kufikia kiwango cha chini kabisa kuwahi kuonekana katika kipindi cha miaka saba.

Uchunguzi uliofanywa na shirika la Business Confidence Index, umeonyesha kiashirio cha biashara kimeshuka kwa ponti 19 kufikia pointi 48, kiwango ambacho kinaelezwa kuwa cha chini tangu mwaka wa 1988. Uchunguzi huo pia umeonyesha kuwa viwango vya riba, sheria kali za mikopo, upungufu wa umeme na mfumuko mkubwa wa bei, yote hayo yameviathiri viwango vya biashara nchini Afrika Kusini.