Kamati ya Nobel yatangaza washindi wa tuzo ya amani
8 Oktoba 2021Washindi hao wametangazwa leo Ijumaa na Berit Reiss Andersen, mwenyekiti wa kamati ya Nobel ya nchini Norway.
Akitangaza washindi hao, Reiss Andersen amesema uandishi huru na unaozingatia ukweli unasaidia kulinda dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka, uongo na propaganda za kivita. Bila uhuru wa kujieleza na uhuru wa habari, Reiss-Andersen amesema, itakuwa vugumu kukuza kwa ufanisi, udugu baina ya mataifa, upunguzaji wa nguvu za silaha na kujenga utaratibu bora wa dunia katika zama zetu.
Kamati ya Nobel imesema Ressa, mnamo mwaka 2012 alikuwa mwasisi mwenza wa mtandao wa habari wa Rappler, ambao umekuwa msitari wa mbele kukosoa kampeni tata na kikatili ya rais wa Ufilipino Rodrigo Durtete, ya kupambana dhidi ya madawa ya kulevya.
Yeye na Rappler, wameandika pia namna mitandao ya kijamii inatumika kusambaza habari za uzushi, kuwanyanyasa wapinzani na kuupotosha umma.
Kwa upande wake, Muratov alikuwa mmoja wa waanzilishi wa gazeti huru la Urusi la Novaya Gazeta mnamo mwaka 1993. Gazeti hilo ndiyo huru zaidi nchini Urusi hii leo, likiwa na mtazamo wa ukosoaji kwa mamlaka, imesema kamati ya Nobel.
Soma pia: Mtanzania Abdulrazak Gurnah ashinda nishani ya Nobel ya Fasihi
Imeongeza kuwa uandishi wa gazeti hilo unaozingatia ukweli na ueledi vimelifanya kuwa chanzo muhimu cha taarifa kuhusu masuala yanayokosolewa ya jamii ya Urusi ambayo ni nadra kutajwa na vyombo vingine.
Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov, amempongeza Muratov kwa ushindi wa tuzo hiyo, na kumsifu kama mtu mwenye kipaji na jasiri.
Tuzo ya Nobel inalenga kutambua mtu au mashirika ambayo yanafanya kazi bora au kubwa zaidi kwa ajili ya kujenga maridhiano baina ya mataifa.
Uandishi huru unasaidia kulinda dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka
Tuzo ya mwaka jana ilikwenda kwa shirika la chakula duniani WFP, ambalo lilianzishwa mwaka 1961 kwa agizo la rais wa Marekani Dwight Eisenhower ili kukabiliana na njaa kote duniani. Shirika hilo lenye makao yake mjini Rome Italia, lilisifiwa kwa juhudi zake za kukomesha matumizi ya njaa kama silaha ya kivita na mizozo.
Tuzo hiyo ya kifahari inaambatana na nishani ya dhahabu na pesa taslimu zaidi ya dola za Marekani milioni 1.4. Zawadi ya pesa hiyo inatoka kwenye urithi ulioachwa na muasisi wa tuzo hiyo, mvumbuzi wa Sweden Alfred Nobel, aliefariki mwaka 1895.
Jumatatu wiki hii, kamati ya Nobel ilitoa tuzo ya fiziolojia au utabibu kwa Wamarekani David Julius na Ardem Patapoutian, kutokana na ugunduzi wao juu ya namna mwili wa binadamu unatambua joto na mguso.
Soma pia: Mwanaharakati mshindi mbadala wa Tuzo ya Nobel
Tuzo ya Nobel katika fizikia ilitolewa Jumanne kwa wanasayansi watatu ambao kazi yao iligundua nidhamu katika hali inayoonekana kukosa nidhamu, na hivyo kusaidia kufafanua na kutabiri nguvu ngumu za kiasili, ikiwemo ufahamu wetu unaopanuka kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Benjamini List na David W.C MacMillan ndiyo walitunzwa nishani ya kemia Jumatano kwa kugundua njia safi zaidi na rafiki wa mazingira ya kujenga molekyula zinazoweza kutumika kutengeneza mchanganyiko, ikiwemo dawa za kutibu na za kuulia wadudu.
Tuzo ya Nobel katika fasihi ilitolewa jana kwa mwandishi wa Kitanzania mwenye makao yake nchini Uingereza Abdulrazak Gurnah, kwa kutambua kazi zake juu ya athari za ukoloni na hatima ya mkimbizi. Siku ya Jumatatu itatolewa tuzo ya kutambua kazi ya kipekee katika nyanja ya uchumi.