Mtanzania Gurnah ashinda nishani ya Nobel ya Fasihi
7 Oktoba 2021Gurnah ambaye alikulia katika visiwa vya Zanzibar lakini akawasili Uingereza kama mkimbizi mwishoni mwa miaka ya 1960, ndiye mwafrika wa tano kushinda nishani ya Nobel ya fasihi.
Chuo cha Sweden kimesema Gurnah ametambuliwa kwa kazi zake mashuhuri zinazoangazia athari za ukoloni na hatima ya mkimbizi katika ghuba kati ya tamaduni na mabara.
Wakfu wa Nobel umesema riwaya zake zinereja nyuma kutoka maelezo ya upotoshaji na kutufungua macho kuhusu kanda yenye uanuwai wa kitamaduni ya Afrika Mashariki ambayo kwa wengi katika maeneo mengine ya dunia haifahamiki.
Gurnah, ambaye alistafu hivi karibuni kama profesa wa fasihi ya bada ya ukoloni katika chuo kikuu cha Kent, alipata simu kutoka Chuo cha Sweden akiwa jikoni nyumbani kwake kusini-mashariki mwa England.
Ameiambia tovuti ya Tuzo ya Nobel kwamba amepatwa na mshangao baada ya kupokea simu hiyi, na akifikiri kuwa ilikuwa ni mzaha.
Mkuu wa kamati ya Nobel ya Chuo cha Sweden, Anders Olsson, amesema mawazo ya Gurnah kuhusu madhila ya wakimbizi yalikuwa yanaenda sawia na wakati huu.
Soma pia: Mtanzania Abdulrazak Gurnah ashinda tuzo ya Nobel ya Fasihi
"Wahusika wa Gurnah nchini Uingereza au barani Afrika wanajikuta katika shimo kubwa kati ya tamaduni na mabara, kati ya maisha yaliyoachwa nyuma na maisha yajayo, wakikabiliana na ubaguzi wa rangi na ubaguzi lakini pia wanajilazimisha kunyamazisha ukweli au kubuni upya wasifu ili kuepuka kupingana na uhalisia. "
Gurnah ambaye amezaliwa mwaka 1948 visiwani Zanzibar, nchini Tanzania, alihamia Uingereza kama mkimbizi mtoto mwaka 1968, akikimbia utawala wa kikandamizaji uliowatesa watu wa jamii ya Waislamu wa Kiarabu ambao yeye alikuwa sehemu yao.
Amesema alianza kuandika baada ya kuwasili England, kama njia ya kuchunguza hasara na pia ukombozi wa uzoefu wa uhamiaji.
Gurnah ndiye mwandishi wa riwaya 10, zikiwemo "Memory of Departure," au "Kumbukumbu ya Kuondoka", "Pilgrims Way" au Njia ya Mahujjaji," na "Paradise" au "Pepo", zilizoorodheshwa kushindania tuzo ya Booker mnamo mwaka 1994, na" By Sea" - Kwa njia ya Bahari na "Desertion," "Utoro".
Soma pia: Tuzo ya Nobel ya Fasihi haitotolewa mwaka huu
Nyingi ya kazi zake zinachungua kile alichokiita, "moja ya simulizi ya nyakati zetu": Ambayo ni athari pana ya uhamiaji juu ya watu waliofurushwa na maeneo wanayofanya kuwa makaazi yao mapya.
Gurnah ambaye lugha yake ya mama ni Kiswahili lakini anaandika katika Kiingereza, ndiye mzaliwa wa sita wa Afrika kutunukiwa nishani ya Nobel ya Fasihi, ambayo imehodhiwa kwa sehemu kubwa ya raia wa wandishi wa Ulaya na Amerika Kaskazini tangu ilipoasisiwa mwaka 1901.
Chanzo: Mashirika