Wauguzi 16 Kenya wapoteza maisha kutokana na COVID-19
18 Septemba 2020Wizara hiyo imeeleza kuwa wauguzi wanakabiliwa na hatari ya maambukizi ya magonjwa mengine pamoja na mashambulizi na unyanyapaa wanapowahudumia wagonjwa wa COVID-19. Kwenye ujumbe wake wa maadhimisho ya siku ya kutambua usalama wa wagonjwa ulimwenguni mwaka huu, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesisitiza kuwa ni muhimu kuzingatia usalama wa wauguzi ili kuwaweka wagonjwa salama.
''Mmoja kati ya wagonjwa 10 wanaolazwa hospitalini hupitia huduma isiyo salama. Hili ni tatizo kwa mataifa yote, mataifa tajiri na yale masikini. Njia mojawapo ya kuwaweka wagonjwa salama ni kwa kuwaweka wauguzi salama. Janga la COVID-19 limetukumbusha sisi sote kuhusu jukumu muhimu wanalotekeleza wauguzi katika kutibu na kuyaokoa maisha,'' alisema Tedros.
Wizara ya afya nchini Kenya imesema katika kipindi cha kati ya mwezi Machi hadi sasa wauguzi 945 wameambukizwa ugonjwa wa COVID-19, na 16 kati yao wamepoteza maisha. Katibu Mkuu wa wizara ya afya Dokta Mercy Mwangangi ameeleza kwamba wanapokuwa kwenye mstari wa mbele kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona, wauguzi wanakabiliwa na hatari ya kuambukizwa magonjwa kama vile homa ya manjano, kifua kikuu na virusi vya ukimwi.
''Wauguzi 16 wamefariki kutokana na ugonjwa wa COVID 19 kutoka kaunti 35 nchini. Tunatambua mchango mkubwa wa wauguzi nchini, tunafahamu umuhimu wa usalama wao na tunawashukuru kwa kazi njema,'' alifafanua Mwangangi.
Ingawaje serikali ya Kenya imekariri msimamo wake wa kuhakikisha wauguzi wamelindwa wakati huu, hali ya utendaji kazi katika mazingara magumu inaendelea kuwakabili. Katika kaunti mbalimbali miungano ya wauguzi bado inaishinikiza serikali kuwalipa mishara na marupurupu yao, baadhi wakidai tangia mwezi Julai mwaka huu. Daktari Mwachonda Chibanzi ni kaimu katibu mkuu wa muungano wa kitaifa wa wauguzi na wadaktari.
''Kwa nini tunateseka kiasi hiki, kama wafanyakazi na kama Wakenya? Hatupokei huduma tunazohitaji ilhali kuna uongozi katika nchi hii,'' alisema Chibanzi.
Hata hivyo, baadhi ya mashirika ya kijamii na kampuni wametambua mchango wa wauguzi na kuchukua hatua mbalimbali za kuwapa motisha. Mjini Nakuru hoteli moja imejitolea kutoa chakula kwa zaidi ya wauguzi 50 wanapokuwa kazini.
Wizara afya nchini imeeleza kuwa wauguzi wanapowahudumia wagonjwa wa COVID 19 wanapitia mashambulizi kutoka kwa wagonjwa hao, msongo wa mawazo na hata unyanyapaa kutoka kwa jamii.