1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Janga la Covid-19 labisha hodi hospitali ya wazazi Nairobi

Shisia Wassilwa15 Julai 2020

Wahudumu wa afya katika Hospitali ya wazazi ya Pumwani jijini Nairobi wameanza mgomo baridi, baada ya wafanyakazi wake 41 kuambukizwa virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3fLjA
Kenia Pumwani Maternity Krankenhaus
Picha: DW/S. Wasilwa

Idadi kubwa ya wafanyakazi katika hospitali kubwa ya umma ya kujifungulia kina mama wajawazito ya Pumwani, wameonesha wasiwasi mkubwa, wakisema kuwa wanalazimishwa kuhudumu licha ya hali kuwa mbaya na mazingira mabovu ya kazi.

Hali ya taharuki, imekikumba kituo hicho huku uongozi wake ukihofia, kuendelea kupima na kutoa matokeo ya uchunguzi wa virusi vya corona. Kaimu mkurugenzi wa idara ya Afya Patrick Amoth, ametaja idadi ya wahudumu wanaougua huku akifafanua kuwa wahudumu walioasalia watapimwa kubaini hali yao.

‘'Wahudumu wa afya wamepatikana na virusi vya Corona, tunaangalia jinsi hospitali hii, ilivyojitayarisha na pia kuweka mikakati ya kukabiliana na ugonjwa wenyewe wakati huu,'' alisema Amoth.

Amoth alisema kuwa wahudumu hao 41, ni miongoni mwa wengine 290 waliopimwa. Wafanyakazi wanahudumu kwa wasiwasi, wasijue kiwango cha usambaaji wa ugonjwa huo na kuwaweka hatarini kina mama waliojifungua na watoto wao.

Kenia Corona-Pandemie
Chama cha wahudumu wa afya nchini Kenya kimewataka wanachama wake kususia kazi hadi serikali itakapoweka vifaa vya kinga. Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Inganga

Katibu Mkuu wa chama cha wauguzi Alfred Obengo ameikosoa hospitali hiyo kwa kuhatarisha maisha ya wafanyakazi wake, na kuongeza kuwa serikali haiwezi kulaumiwa wakati huu lakini, uongozi wa hospitali hiyo ndiyo unastahili kunyooshewa kidole cha lawama.

‘'Mkuu wa wauguzi na msimamizi wa hospitali, hawana uzoefu wa kukabiliana na covid-19, wanastahili kujibu na kuwajibika vilivyo,'' alisema Obengo.

Chama hicho sasa kinaitaka serikali kuboresha mazingira ya utendajikazi, kwa kuwapa wafanyakazi vifaa vinavyostahili kukabiliana na makali ya Covid-19.

Hayo yanajiri wakati taifa likiomboleza kifo cha kwanza cha daktari aliyeaga dunia kutokana na ugonjwa huo siku chache zilizopitwa.

Kwa mujibu wa wizara ya Afya jumla ya wahudumu 429 wa afya kote nchini Kenya, wameambukizwa virusi vya corona tangu mwezi Machi. Visa vya ugonjwa huo vimekuwa vikiongezeka siku baada ya nyingine.

Iwapo hali itazidi kuwa hivyo, huenda serikali ikabana masharti na kufunga mipaka ya majimbo kama ilivyokuwa miezi mitatu iliyopita. Tayari visa 10000 vya ugonjwa huo vimeripotiwa katika taifa la Kenya.