1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za suluhu Sudan, zaendelea

2 Novemba 2021

Juhudi za kusaka uwezekano wa kupatikana kwa suluhu ya kisiasa ndani na nje ya Sudan zinaendelea ikiwa ni wiki moja baada ya serikali ya kiraia kupinduliwa na jeshi.

https://p.dw.com/p/42Spj
USA New York | UN Hauptquartier - Voler Perthes zu Sudan
Picha: Loey Felipe/Xinhua/picture alliance

Akizungumza kwa njia ya video kutokea Khartoum, mjumbe wa Umoja wa Mataifa Volker Perthes amewaambia waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja huo mjini New York kwamba mazungumzo yanaendelea baina yao na wajumbe wa ndani, kikanda na kimataifa ambao kwa pamoja wanaelezea nia yao thabiti ya juhudi hizi kusonga mbele haraka ili kujiondoa kwenye mzozo huo na kurejea katika hali ya kawaida.

Mjumbe huyo aidha alirejea tena kutoa mwito wa kuachiwa kwa wafungwa kama moja ya njia ya keuelekea kwenye maridhiano na kuondoa ukandamizaji.

"Tumeshuhudia mawimbi kadhaa ya kamatakamata baadhi ya viongozi wa kisiasa wanazuiwa, wanaharakati na marafiki wanaopinga mapinduzi haya bado wanakamatwa. Ni kwa maana hiyo basi ndio maana nimekuwa nikitoa mwito mara kwa mara kwa mamlaka kuwaachia huru wafungwa," amesema mjumbe huyo.

Soma Zaidi: Kamata kamata yaendelea Sudan baada ya mapinduzi

Jana Jumatatu mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa aliitole mwito Sudan kurejea kwenye mchakato wa mabadilishano ya kisiasa ambao ulikuwa ukishuhudiwa kabla ya mapinduzi hayo ya kijeshi ya Oktoba 25. Siku ya Jumapili alikutana na waziri mkuu aliyeondolewa mamlakani Abdallah Hamdok ambaye bado anazuiwa kwenye kifungo cha nyumbani na baadae kuandika kwenye ukurasa wake wa twitter kwamba majadiliano bado yanaendelea.

Putsch im Sudan | General Abdel Fattah al-Burhan
Kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan anakosolewa vikali dhidi ya mapinduzi hayo.Picha: /AP/dpa/picture alliance

Oktoba 25, Jenerali wa juu wa Sudan Abdel Fattah al-Burhan alilivunja baraza la mawaziri pamoja na baraza la pamoja la kijeshi la kiraia lililokuwa likiongoza taifa hilo katika kipindi cha mpito baada ya kuondolewa kwa aliyekuwa kiongozi wa kiimla kwenye taifa hilo Omar al-Bashir mnamo mwaka 2019.

Kwenye mapinduzi hayo ambayo yalikosolewa vikali na jumuiya ya kimataifa, Burhan alitangaza hali ya dharura na kuwazuia viongozi wa serikali ya kiraia, ikiwa ni pamoja na waziri mkuu Hamdok ingawa baadaye aliachiwa huru na kuwekwa chini ya kifungo cha nyumbani.

Ubalozi wa Marekani nchini humo umesema jana kwamba hali imeendelea kuimarika hasa baada ya maandamano yaliyofanyika siku ya Jumamosi, lakini hata hivyo bado kuna vizuizi vya kijeshi vya ukaguzi katika baadhi ya maeneo na waandamanaji nao wakiendelea kuweka vizuizi vinavyohamishika katika baadhi ya maeneo kote katika mji wa Khartoum.

Aidha Uingereza hapo jana ilisema kwamba imeliomba shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia haki za binaadamu mjini Geneva kuitisha kikao cha dharura kuhusu Sudan kufuatia mapinduzi hayo ya kijeshi.

Sikiliza Zaidi: 

Sudan yaendelea kusakamwa kufuatia mapinduzi ya kijeshi

Mashirika: AFPE