1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani kwa jeshi la Sudan wazidi

29 Oktoba 2021

Marekani na Umoja wa Mataifa wameliwekea shinikizo jeshi la Sudan wakati ambapo makabiliano kati ya wanajeshi na waandamanaji wanaopinga mapinduzi yamepelekea idadi ya waliofariki kufikia watu 11.

https://p.dw.com/p/42L2C
Sudan Karthoum | Proteste gegen den Militärputsch
Picha: EBAID AHMED/REUTERS

Baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa wito wa kurudishwa kwa serikali ya kiraia nchini Sudan iliyopinduliwa Jumatatu wiki hii na jenerali Abdel Fattah al-Burhan, Rais wa Marekani Joe Biden amesema nchi yake kama nchi zengine inasimama na waandamanaji.

Huku maelfu wakiingia mitaani kuandamana, mashuhuda wanasema risasi za mpira na zile za moto zilitumika ili kuwatawanya waandamanaji mnamo wakati maandamano ya kila usiku yanapopamba moto.

Nach Militärputsch im Sudan
Waandamanajin wakikabiliana na maafisa wa usalamaPicha: AFP

Majadiliano ya kumchagua waziri mkuu yanaendelea

Kamati ya madaktari inayofuatilia machafuko hayo imesema mtu mmoja ameuwawa na wawili wengine kujeruhiwa vibaya. Duru za kitabibu zinaeleza kwamba mapema Alhamis mtu mmoja mwenye umri wa miaka 22 alifariki dunia kutokana na majeraha ya risasi na kupelekea idadi ya waliofariki kufikia watu 11.

Usiku wa kuamkia Ijumaa video ya Burhan iliyoonyeshwa na shirika la habari la Al Jazeera imemuonyesha jenerali huyo akisema kwamba majadiliano yanaendelea ili kumchagua waziri mkuu.

Wafanyakazi wakuu wa serikali wakiwemo mabalozi wa Sudan, makundi na taasisi zengine wamelaani hatua ya kamanda huyo mkuu. Wizara ya utamaduni na mawasiliano ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuonyesha upinzani kwa hatua hiyo kwa kuandika ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa Facebook.

Alhamis serikali ndogo ya mji wa Khartoum iliongeza sauti yake katika mapinduzi yaliyofanyika licha ya kuwa gavana alikuwa mmoja wa waliokamatwa na Burhan. Taarifa iliyotiwa saini na wakuu wa serikali hiyo imelaani mapinduzi hayo na kusema Sudan haitorudi katika udikteta uliopita. Taarifa hiyo pia iliunga mkono maandamano yanayofanywa na raia na kutaka waandamanaji wapewe bidhaa muhimu kama unga na madawa ya dharura.

Mabalozi wafutwa kazi kwa kulipinga jeshi

Wanadiplomasia pia wamekuwa miongoni mwa wanaopinga hatua hiyo huku baadhi ya mabalozi wa Sudan wakisema hadharani kwamba wanaunga mkono maaindamano huku wengine wakielezea maoni yao kwa njia ya maandishi.

Sudan |  Abdel Fattah Abdelrahman al-Burhan
Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman al-BurhanPicha: Mahmoud Hjaj /AA/picture alliance

Ali Ibn Abi Talib Abdelrahman Mahmoud ni balozi wa zamani wa mpango wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva.

"Natangaza waziwazi kwamba sitautambua uamuzi wa kiongozi wa mapinduzi ambao kwa usiku mmoja uliiondoa mamlakani serikali halali kikatiba," alisema Abdelrahman.

Burhan amejibu kwa kuwaachisha kazi baadhi ya mabalozi wa nchi hiyo wakiwemo mabalozi wa Sudan nchini China, Ufaransa, Uswisi, Marekani na balozi wa nchi hiyo kwa Umoja wa Ulaya.

Chanzo: Reuters/AFP