1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Judith Suminwa, mwanamke wa kwanza kuwa waziri mkuu Kongo

Jean Noël Ba-Mweze
2 Aprili 2024

Zaidi ya miezi mitatu baada ya kushinda uchaguzi, Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amemteuwa Judith Suminwa Tuluka kuwa mwanamke wa kwanza kuwa waziri mkuu mkuu wa taifa hilo tajiri kwa madini.

https://p.dw.com/p/4eLEB
DR Kongo |  Judith Tuluka Suminwa na Felix Tshisekedi
Waziri Mkuu mpya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Judith Suminwa Tuluka (kushoto), akizungumza na Rais Felix Tshisekedi muda mchache baada ya kuteuliwa kwake, tarehe 1 Aprili 2024.Picha: DRC Presidency/Handout/Xinhua/picture alliance

Mara tu baada ya kutangazwa uteuzi wake siku ya Jumatatu (Aprili 1) Suminwa alipokelewa na Rais Tshisekedi katika Ikulu ya Kinshasa, ambalo aliahidi kufanya kila awezalo kuhakikisha amani inarejea nchini Kongo. 

"Najua majukumu yangu ni makubwa. Nimemuahidi rais kwamba ategemee uaminifu wangu kumsaidia kwa maendeleo ya nchi yetu. Na kuwa  kufuatana na ahadi alizozitoa wakati akiapishwa, tutatumikia amani na maendeleo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo," alisema waziri mkuu huyo mpya.

Soma zaidi: Tshisekedi amteuwa Tuluka kuwa waziri mkuu

Judith Suminwa Tuluka ni mzaliwa wa  mkoa wa Kongo Central ulioko magharibi mwa nchi hiyo na kabla ya wadhifa huu mpya, alishahudumu kama waziri wa mipango kwa muda wa mwaka mmoja chini ya Waziri Mkuu Jean-Michel Sama Lukonde.

Kitaaluma, Suminwa ni mchumi, akiwa na shahada ya uchumi na stashahada ya masomo ya ziada ya usimamizi wa  rasilimali watu katika nchi zinazoendelea na pia ana uzoefu wa kitaaluma katika ngazi za kitaifa na kimataifa.

Mwanamke wa kwanza kuwa waziri mkuu

Judith Suminwa anakuwa mwanamke wa kwanza kuongoza serikali ya Kongo tangu nchi hiyo kupata uhuru wake mwaka 1960.

Felix Tshisekedi wa Kongo
Rais Felix Tshisekedi wakati akiapishwa kwa muhula wa pili tarehe 20 Januari 2024 mjini Kinshasa.Picha: Arsene Mpiana/AFP

"Bi Suminwa tayari amethibitisha ujuzi wake kupitia taaluma yake. Alikuwa waziri mwenzangu ambaye nilitumika naye kwa utekelezaji wa miradi kama ule wa maendeleo ya maeneo 145 ya Kongo. Ni mradi muhimu ulioongozwa naye. Hivi tumpe baraka zote ili kuiongoza serikali ya jamhuri." Alisema Patrick Muyaya, waziri wa mawasiliano na msemaji wa serikali inayoondoka madarakani.

Soma zaidi: Usalama mashariki mwa Kongo waazidi kuzorota huku kundi la waasi yakijiimarisha

Judith Suminwa ni mmoja wa viongozi wa UDPS, chama cha Rais Tshisekedi akiwa pia mshirika wake wa karibu.

Alikuwa Naibu Mratibu wa Baraza la Ufuatiliaji wa Mikakati ya Rais (CPVS) linalofuatilia na kutathmini utekelezaji wa ahadi za Rais Tshisekedi kwa wananchi wa Kongo wakati wa kusaka kura.

Uteuzi wake umejiri huku hali ya usalama ikiendelea kuwa ya wasiwasi mashariki mwa nchi hiyo, ambako baadhi ya maeneo bado yanadhibitiwa nawaasi wa M23 wanaoshukiwa kuungwa mkono na Rwanda.

Hiyo ndiyo changamoto kubwa inayomsubiri Waziri mkuu Judith Suminwa Tuluka.