1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Hali ya usalama mashariki mwa Kongo yazidi kuzorota

28 Machi 2024

Umoja wa Mataifa umesema hali ya usalama katika eneo la mashariki mwa Kongo lililo na utajiri wa madini imezorota tangu baada ya kukamilika kwa uchaguzi mkuu wa mwezi Disemba.

https://p.dw.com/p/4eDsC
Umoja wa Mataifa New York 2019 | Bintou Keita
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika mzozo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Bintou Keita ameonya juu ya hali inavyozidi kuzorota nchini humoPicha: Li Muzi/Xinhua News Agency/picture alliance

Kulingana na Umoja wa Mataifa, kundi moja la waasi linalofungamanishwa na Rwanda, linazidi kujitanua na kuchukua udhibiti wa maeneo.

Akizungumza katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika mzozo huo wa Kongo Bintou Keita, amesema, jambo limesababisha hali mbaya ya kibinadamu, huku kiasi cha wakimbizi wa ndani kikiongezeka pakubwa.

Mwezi uliopita, Marekani iliyaambia mataifa ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongokwamba, yanastahili kujitenga na hatari ya kuzuka kwa vita baina yao.

Naibu balozi wa Marekani Robert Wood amelaani uvamizi wa waasi wa M23 mashariki mwa Kongo na vile vile amelaani hatua ya jamii ya kimataifa kutolaani vitendo vya Rwanda ambayo ni mchangiaji mkubwa wa majeshi katika vikosi vya Umoja wa Mataifa vya Kulinda amani.