1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Sudan lazidi kupokea shinikizo

5 Novemba 2021

Baraza kuu la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa linafanya kikao cha dharura kuhusu Sudan leo Ijumaa baada ya mapinduzi ya kijeshi kuanza karibu wiki mbili zilizopita.

https://p.dw.com/p/42drH
Putsch im Sudan | General Abdel Fattah al-Burhan
Picha: /AP/dpa/picture alliance

Uingereza, Marekani, Ujerumani na Norway zikiongeza msukumo wa kuagizwa mtaalamu wa kufuatilia hali nchini humo. Haya yanajiri wakati uongozi wa kijeshi hapo jana uliamuru kuachiliwa kwa mawaziri wanne waliokuwa kizuizini. Soma Juhudi za suluhu Sudan, zaendelea

Mjadala wa Baraza la Haki za Kibinadamu unafanyika wakati Umoja Mataifa bado unamtambua balozi wa Sudan wa serikali ya kiraia iliyopinduliwa kama mwakilishi rasmi wa Sudan huko Geneva, na kuibua maswali kuhusu jinsi gani au kama uongozi wa kijeshi wa Khartoum utawakilishwa wakati wa kikao hicho.

soma  Upinzani kwa jeshi la Sudan wazidi

Msukumo wa kuwepo mtaalam wa haki za binadamu unatolewa huku kukiwa na shinikizo la kimataifa kwa jenerali mkuu wa Sudan, Jenerali Abdel-Fattah Burhan, na vikosi vinavyomtii baada ya kuivunja serikali ya mpito na kuwaweka kizuizini baadhi ya maafisa serikali na viongozi wa kisiasa katika mapinduzi ya Oktoba 25.

Siku ya Jumatano nchi hizo nne za Magharibi ziliwasilisha rasimu ya mapendekezo ya suluhisho, na lugha ya mwisho bado ilikuwa inafanyiwa kazi. Msemaji wa Baraza la Haki za Binaadam, Rolando Gomez alisema kuna kifungu kinachopendekeza kuundwa kwa 'ripota maalum' kufuatilia hali ilivyo Sudan kwa mwaka mmoja.

Wakati haya yakijiri utawala wa kijeshi nchini Sudan umeamuru kuachiwa huru kwa mawaziri wanne wa serikali iliyopinduliwa ambao wamekuwa wakishikiliwa tangu jeshi lilipochukua madaraka wiki iliyopita. Wanne hao ni waziri wa mawasiliano, biashara, habari na vijana na waziri wa michezo. somaBurhan awaondoa mabalozi 6 kwa kukosoa mapinduzi Sudan

Shinikizo la Kimataifa

USA Ned Price
Ned PricePicha: Olivier Douliery/AP Photo/picture alliance

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, Ned Price, amesema kwamba Marekani inatazamia jeshi litachukuwa hatua za kuruhusu kurejeshwa kwa ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

"Tunaungana na watu wa Sudan katika kutoa wito wa haki na uwajibikaji kwa ukiukaji wa haki za binadamu na tunawahimiza wanajeshi kuacha kuzima mtandao wa intaneti na kuondoa hali ya hatari. Na kuwaachilia viongozi wote wa kiraia na waliopanga maandamano waliozuiliwa tangu walipochukua madaraka.” alisema Ned Price.

Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu Michelle Bachelet ametaja mapinduzi hayo ya kijeshi kuwa ya kutatanisha sana na kutoa wito kwa vikosi vya jeshi, polisi, na vitengo vya ujasusi kusitisha matumizi mabaya ya nguvu dhidi ya raia ambayo amesema hadi sasa yamesababisha vifo vya takriban raia 13.

Muda mfupi uliopita televisheni ya serikali ya Sudan imetangaza kwamba jeshi la Sudan limefuta bodi zote za makampuni ya serikali na miradi ya kitaifa ya kilimo.

 

Reuters,dpa