Polisi Kenya yapiga marufuku maandamano Nairobi
18 Julai 2024Kauli ya polisi ya kuyapiga marufuku maandamano katikati mwa jiji la Nairobi imetolewa baada ya wiki kadhaa za maandamano ya kuipinga serikali.
Mkuu wa polisi, Kanja Kiricho alisema katika taarifa aliyoitoa Jumatano jioni kuwa jeshi la polisi limepata taarifa za kuaminika za kiitelijensia kuwa, makundi ya uhalifu wa kupangwa yanapanga kuyatumia maandamano yanayoendelea ili kufanya mashambulizi yakiwa ni pamoja na uporaji.
Ameongeza kuwa maandamano hayo pia yamepigwa marufuku katika maeneo yanayozunguka eneo la biashara jijini Nairobi ili kuhakikisha usalama wa umma.
Soma zaidi: IGP Kenya ajiwajibisha kwa vifo vya waandamanaji
Awali, wanaharakati walitoa wito kwa watu kukusanyika Alhamisi katika viwanja vya Uhuru huku polisi wakitanda katikati mwa Nairobi. Wanaharakati hao wanasema kuwa wanataka Rais Ruto aachie ngazi. Pia, wametoa wito wa kutaka mageuzi ili kushughulikia ubadhirifu, na utawala mbovu.
Watu wasiopungua 50 wameuwawa tangu yalipoanza maandamano yanayoongozwa na vijana mwezi mmoja uliopita. Maandamano hayo yalianza kwa kwa kupinga muswada tata wa fedha uliotoa mapendekezo ya kuongeza ushuru lakini yaliendelea licha ya Rais William Ruto kuuondoa na kulivunja baraza la mawaziri.
Mgogoro mkubwa tangu Rais Ruto aingie madarakani
Maandamano hayo yaliyoratibiwa kwa njia ya mtandao bila ya uungwaji mkono kutoka kwa wanasiasa wa vyama vya upinzani, yametengeneza mgogoro mkubwa zaidi katika miaka miwili wa rais Ruto madarakani. Yalianza kwa amani lakini baadaye yalikumbwa na vurugu.
Wiki iliyopita, Rais William Ruto, aliahidi kuunda serikali ya kitaifa lakini muungano wa vyama vya upinzani ulikataa wazo hilo na badala yake unataka utawala unaofuata katiba.
Soma zaid: Shinikizo zaiandama serikali ya Kenya kuwatuliza waandamanaji
Ofisi yake, ilipanga kufanya mazungumzo na sekta mbalimbali wiki hii ili kuyashughulikia manung'uniko ya waandamanaji lakini hadi kufikia Alhamisi, hakukuwa na dalili ya kuanza kwa majadiliano hayo. Wengi wa viongozi wa maandamano wamekataa mwaliko wa ofisi ya Rais Ruto na badala yake wanataka masuala kama rushwa yashughulikiwe haraka.
Katika hatua nyingine, mamlaka ya mawasiliano ya Kenya imevitahadharisha vyombo vya habari dhidi ya kuchochea vurugu katika matangazo yao yanayohusu maandamano. Mamlaka hiyo kupitia Mkuu wake David Mugonyi imesema kufanya hivyo kunaweza kusababisha machafuko ndani ya taifa hilo.