Mahakama Kenya yaidhinisha kutumiwa jeshi kutuliza ghasia
29 Juni 2024Wakati magari ya kivita ya kijeshi yalionekana Alhamisi mjini Nairobi, mahakama ilitoa uamuzi jana jioni kuwa hatua ya kutumiwa jeshi iliyoidhinishwa na bunge, ni ya halali kutokana na kuzuka kwa machafuko wakati wa maandamano, ambayo polisi wameshindwa kuyadhibiti. Mahakama ilipinga rufaa iliyowasilishwa na chama cha wanasheria.
Jumanne wiki hii, waandamanaji walivamia bunge na kuchoma moto sehemu ya jengo hilo. Hata hivyo Jaji Lawrence Mugambi pia alionya kuhusu kile alichosema mwenendo hatari ambao huenda ukasababisha nchi kuwa chini ya udhibiti wa jeshi. Kwa hiyo ametaka taarifa sahihi kutoka kwa serikali katika siku mbili kuhusu upeo na muda wa operesheni hiyo.
Soma pia: Blinken akaribisha hatua za rais wa Kenya kutuliza mvutano
Alhamisi kulishuhudiwa maandamano katika maeneo tofauti ya nchi ukiwemo mji mkuu Nairobi. Kulikuwa na ulinzi mkali hasa katika eneo la Ikulu baada ya waandamanaji kusema walipanga kuandamana hadi Ikulu ya Rais.