1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Vifaru na wanajeshi wa Israel wavamia kwa muda Gaza

27 Oktoba 2023

Wanajeshi wa Israel pamoja na vifaru walilivamia kwa muda eneo la kaskazini mwa Gaza usiku wa kuamkia jana Alhamisi na kupambana na wapiganaji wa Hamas.

https://p.dw.com/p/4Y5Ak
Vifaru vya jeshi la Israel vikiwa karibu na Ukanda wa Gaza Oktoba 12, 2023
Vifaru vya jeshi la Israel vikiwa karibu na Ukanda wa Gaza Oktoba 12, 2023Picha: Mostafa Alkharouf/AA/picture alliance

Taarifa zinasema, wanajeshi walipambana na wapiganaji wa Hamas ili kuandaa kile walichosema "uwanja wa vita" kabla ya operesheni yake ya ardhini, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari katika ukanda wa video.

Soma zaidi:UN: Hakuna mahali palipo salama huko Gaza

Benny Gantz, jenerali mstaafu na mjumbe wa Baraza maalumu la mawaziri la vita la Israel kwa upande wake amesema mashambulizi hayo ya ardhini yatakuwa ni hatua moja miongoni mwa nyinginezo katika mchakato wa muda mrefu utakaojumuisha masuala ya usalama, siasa na kijamii nchini Israel.

Raia 250,000 wa Israel waondoka kwa hiyari Gaza

Viongozi mbalimbali wamekuwa wakitoa matamshi ya kupinga mashambulizi hayo ambayo Israel inajiandaa kuyafanya katika Ukanda wa Gaza, kwa hofu kwamba yatawadhuru raia wasio na hatia waishio kwenye eneo hilo. Jeshi la Israel limearifu kwamba tayari raia 250,000 wa Israel wameondoka kwa hiyari kuepuka mapigano katika maeneo yaliyo karibu na mpaka wa Gaza na pia mashambulizi ya maroketi kwenye mpaka wa kaskazini baina ya Israel na Lebanon. 

Afisa mwandamizi wa Hamas Musa Abu Marzook ni miongoni mwa maafisa wa Hamas wanaohudhuria mazungumzo mjini Moscow
Afisa mwandamizi wa Hamas Musa Abu Marzook ni miongoni mwa maafisa wa Hamas wanaohudhuria mazungumzo mjini MoscowPicha: Sefa Karacan/AA/picture alliance

Katika hatua nyingine, ujumbe wa Hamas umeelekea Moscow jana Alhamisi kwa ajili ya mazungumzo yanayohusiana na kuwaachia mateka wa kimataifa, ambao ni pamoja na raia wa Urusi, hii ikiwa ni kulingana na mashirika ya habari ya Urusi yaliyonukuu wizara ya mambo ya nje ya Urusi.

Afisa mwandamizi wa Hamas Abu Marzouk ni miongoni mwa wanaoshiriki kwenye mazungumzo hayo, limesema shirika la habari la Urusi, TASS.

Urusi mara kwa mara imesema mzozo huu wa sasa umechochewa na kushindwa kwa sera za kigeni za Marekani huku ikitoa mwito wa kusitishwa mapigano na kuanza mazungumzo ili kupata suluhu ya amani. Israel imekosoa ziara hiyo na kuiomba Urusi kuufukuza ujumbe huo wa Hamas na kuongeza kuwa wamesikitishwa na hatua hiyo ya kuwakaribisha Moscow.

Wizara ya mambo ya nje ya Israel imesema Hamas ni kundi la kigaidi linalofanya vitendo vibaya zaidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu na kwamba mikono ya maafisa waandamizi wa Hamas imejaa damu ya zaidi ya Waisrael 1,400 lakini pia utekaji wa zaidi ya Waisrael 220.

Palestina yaomba Umoja wa Mataifa kutambua mateso wanayoyapitia Wapalestina

Huku hayo yakijiri, kikao cha dharura cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kinafanyika mjini New York. Katika kikao hicho, balozi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa Riyad Mansour ametoa wito kwa baraza hilo kutambua "mateso makubwa" yanayowakumba Wapalestina huko Gaza.

Mwakilishi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa Riyad Mansour ameuomba Umoja huo kuyatambua mateso yanayowakabiliwa Wapalestina
Mwakilishi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa Riyad Mansour ameuomba Umoja huo kuyatambua mateso yanayowakabiliwa WapalestinaPicha: John Angelillo/newscom/picture alliance

Mansour amesema karibu Wapalestina 7,000 wameuawa katika mashambulizi ya Israel, baada ya shambulizi la Hamas la Oktoba 7.

Naye balozi wa Israel kwenye Umoja huo wa Mataifa Gilard Edan aliposimama kuzungumza alisema Israel haipigani na Wapalestina lakini inakabiliwa na kundi la kigaidi linalofanya mauaji ya kimbari la Hamas. Amesema Hamas haiwajali watu wa Palestina wala haina mpango wa amani.

Muswada wa suluhu unaotoa wito wa kusitisha mapigano uliowasilishwa na Jordan utapigiwa kura mwishoni mwa kikao hicho. Hata hivyo kuna mashaka makubwa iwapo muswada huo utaidhinishwa.

Na huko Brussels, viongozi wa Umoja wa Ulaya wametoa wito wa kusimishwa kwa mapigano na kufunguliwa kwa njia za kiutu ili misaada iingie Gaza baada ya majadiliano ya masaa kadhaa katika mkutano wa kilele wa umoja huo.

Soma zaidi:Borrell aunga mkono kusitishwa mapigano ili kuruhusu misaada kuingia Gaza

Sehemu ya taarifa yao imesema Baraza la Ulaya linaelezea wasiwasi wake mkubwa kutokana na kudhoofika kwa mazingira ya kiutu huko Gaza na kutoa wito wa njia za kufikisha misaada ya kibiaadamu ziendelee kuwa wazi na bila ya vizuizi ili kuwafikia haraka uwanaouhitaji.