Biden aifananisha Hamas na Putin katika hotuba yake
20 Oktoba 2023Katika hotuba yake ya nadra kwenye ofisi ya Rais, maarufu kama Oval Room, Biden amesema ikiwa alichokiita "uchokozi wa kimataifa" kitaruhusiwa kuendelea, basi kuna hatari ya migogoro na machafuko kuweza kuenea katika sehemu nyingine za ulimwengu. Biden amelifananisha kundi la Hamas na Putin akisema kuwa wanawakilisha vitisho tofauti lakini wanafanana kwa azma ya kuangamiza taifa jirani la kidemokrasia.
Alichosema Biden katika ziara yake Israel: Biden: Nimechukizwa na shambulio la hospitali Gaza
Aidha rais huyo amesisitiza kwamba ushindi wa Israel na Ukraine katika vita vyao ni suala lenye umuhimu mkubwa kwa usalama wa Washington. Hii leo, Biden atawasilisha ombi la dola bilioni 100 za ufadhili wa dharura. Sehemu kubwa ya ufadhili huo itaelekezwa katika vita vya Ukraine. Fedha nyingine ni kwa ajili ya Israel pamoja na ulinzi katika eneo la Indo-Pacific.
Mapigano yaendelea Gaza
Israel imeendeleza mashambulizi ya angani kuelekea ukanda huo huku waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant akiviamuru vikosi vya nchi hiyo vilivyoko mpakani kujitayarisha kwa ajili ya mashambulizi ya ardhini. Akizungumza na wanajeshi wa Israel, Gallant amedai hivi karibuni wataweza "kuiona Gaza kutokea ndani".
Mashambulizi hayo ya angani mapema siku ya Alhamis yalielekezwa katika maeneo yote ya Gaza, ikiwemo maeneo ya kusini ambayo Israel iliyatangaza kuwa salama. Zaidi ya Wapalestina milioni moja ambao ni takribani nusu ya wakaazi wa Gaza, wameyakimbia makaazi yao kaskazini mwa mji huo baada ya Israel kuwataka waondoke.
Wizara ya afya inayoendeshwa na kundi la Hamas, katika taarifa yake imedai kwamba Wapalestina wapatao 3,785 wameuawa na wengine karibu 12,500 wamejeruhiwa. Zaidi ya Waisrael 1,400 wameuawa, katika shambulio la Hamas la Oktoba 7. Hamas inachukuliwa na nchi za magharibi kama Marekani na Umoja wa Ulaya kuwa kundi la kigaidi.
Misaada ya kiutu.
Misri inajiandaa kuruhusu misaada kupitia kivuko cha mpaka wake na Gaza huku usafirishaji wa kwanza ukitarajiwa leo Ijumaa. Kivuko hicho cha Rafah hakijafanya kazi tangu kuanza kwa vita hivi..
Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amehimiza "ufikiaji wa haraka na usiozuiliwa wa misaada ya kibinadamu" kwenye Ukanda wa Gaza uliozingirwa, wakati Israeli ikiendeleza mashambulizi yake dhidi ya Hamas. Guterres ameyasema hayo akiwa mjini Cairo, Misri, wakati miito ya usambazwaji wa misaada ya kiutu ikizidi kuongezeka ili kulifikia eneo hilo lenye raia wapatao milioni 2.4.
Katika mkutano wa pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Misri, Sameh Shoukry, Guterres ametoa wito wa "usitishaji wa haraka wa mapigano kwa ajili ya misaada ya kibinaadamu".
Makubaliano ya kuruhusu misaada: Israel na Misri zaruhusu misaada ya kibinaadamu kupelekwa Gaza
Mkuu wa masuala ya misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths anakadiria kwamba malori yapatayo 100 kwa siku yanahitajika ili kukidhi mahitaji ya Gaza.
Wakati huo huo, Misri inaandaa mkutano wa kilele wa amani utakaofanyika kesho Jumamosi, kwa madhumuni ya kujaribu "kupunguza mapigano" pamoja na "kuhakikisha usambazwaji wa misaada ya kibinaadamu".
Juhudi za diplomasia
Kwa upande mwengine, mawaziri wawili wa Ujerumani, waziri wa mambo ya nje Annalena Baerbock na waziri wa ulinzi Boris Pistorious, waliwasili jana Mashariki ya Kati na kusisitiza uungwaji mkono kwa Israel.
Soma pia: China yatoa wito wa kusitishwa vita vya Gaza
Pistorius alikutana na mwenzake wa ulinzi wa Israel, Yoav Gallant, na kusema jukumu la dharura zaidi ni kufanikisha kuachiliwa kwa zaidi ya watu 200 wanaoshikiliwa mateka na Hamas huko Gaza.
Baerbock, kwa upande wake alikuwa mjini Amman Jordan, na kukutana na kamishna mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, Philippe Lazzarini, kujadili hali mbaya ya kibinadamu huko Gaza.
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak naye pia alizuru Israelna kuonyesha mshikamano na taifa hilo. Baadaye alielekea Saudi Arabia na kukutana na Mwanamfalme Mohammed bin Salman ambaye amemueleza Sunak kwamba suala la kuwalenga raia huko Gaza ni "uhalifu mkubwa".
Na familia za baadhi ya watu waliotekwa zimetoa wito kwa kundi la Hamas kuwaachilia huru jamaa zao na kuwataka wanajeshi wa Israel kuzingatia usalama wao wakati wakipambana na kundi hilo. Raia wa kigeni ni miongoni mwa watu waliouawa, kujeruhiwa au kuchukuliwa mateka na Hamas mnamo Oktoba 7.
Kulingana na takwimu za shirika la habari la AFP, karibu wageni 200 wamethibitishwa kufariki, wengi wao pia wakiwa na uraia wa Israel. Raia wa Ujerumani ni miongoni mwa mateka.