Israel yashambulia kusini kwa Gaza
19 Oktoba 2023Mashambulizi hayo yamefanyika hata baada ya Israel kukubali siku ya Jumatano (Oktoba 18) kuiruhusu Misri kupeleka msaada kiasi wa kibinaadamu mjini Gaza, siku 12 tangu ianze kuushambulia ukanda huo na kutangaza mzingiro kamili.
Tangazo la mpango wa kupeleka chakula, maji na mahitaji mengine Gaza limekuja wakati hasira juu ya shambulio baya dhidi ya hospitali mjini Gaza, zikienea kote Mashariki ya Kati.
Soma zaidi: Israel na Hamas zaendelea kushambuliana Ukanda wa Gaza
Rais Joe Biden wa Marekani amerejea Washington baada ya kuizuru Israel siku ya Jumatano katika kile kinachosemwa ni "kujaribu kuzuwia kusambaa kwa mzozo huo."
Watu 3,478 wameuawa mjini Gaza, na zaidi ya 12,000 kujeruhiwa, huku wengine 1,300 wanaaminika kufunikwa na vifusi kulingana na maafisa wa afya wa Gaza tangu Israel ilipoanza operesheni ya kijeshi Oktoba 7.
Kwa upande wake Israel, imeripoti vifo zaidi ya 1,400, na wengine watapato 200 walichukuliwa mateka na wanamgambo wa Hamas baada ya uvamizi wa kundi hilo, ambalo linatambuliwa na Marekani na Umoja wa Ulaya kuwa kigaidi.