DRC yaishutumu Rwanda kupanga kuishambulia
28 Julai 2023Kauli hiyo ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imetolewa, ikiwa ni ishara ya kuongezeka kwa mvutano kati ya taifa hilo na Rwanda.
Katika kauli yake, msemaji wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jenerali Sylvain Ekenge amesema kwamba mapema Alhamisi, wanajeshi wa Rwanda walivuka mpaka kaskazini mwa Goma katika kile alichokiita kuendelea kuyumbisha na kukiuka kwa makusudi uadilifu wa Kongo.
Soma zaidi:Rwanda yaionya DRC dhidi ya uchokozi
Aliongeza kuwa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo lilifanikiwa kupambana na kuvirudisha nyuma vikosi vya Rwanda akiongeza kuwa nchi yake sasa itajibu mashambulizi kwa nguvu, pigo hadi pigo na kuitumia vilivyo haki yake ya kufuatilia.
Vyanzo viwili vya jeshi vya mjini Goma vilizungumza na shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotajwa majina vikisema kuwa mwanajeshi mmoja wa Rwanda alikufa kutokana na mapambano. Jeshi na serikali ya Rwanda haikutoa maoni yoyote kuhusu tukio hilo ilipoombwa kufanya hivyo na shirika hilo la habari.
Kulingana na takwimu za ofisi ya uratibu wa masuala ya kiutu ya shirika la Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu milioni moja wamelazimika kuyahama makazi yao tangu waasi wa M 23 walipoanza tena mapambano.Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa ikilituhumu taifa jirani la Rwanda kwa kuwaunga waasi wa M23, ambao walianza mapigano mwishoni mwa mwaka 2021 baada ya miaka mingi ya utulivu.
Wapiganaji wa M23 wameyaweka kwenye himaya yao maeneo kadhaa ya Kivu kaskazini, na mnamo mwezi Mei Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo iliituhumu Rwanda kwa kupanga kufanya mashambulizi katika mji mkuu wa mkoa huo.
Makundi ya wabeba silaha yamekuwa tatizo katika sehemu kubwa ya mashariki mwa Kongo kwa miongo kadhaa, yakiwa ni matokeo ya vita vya kikanda vilivyoibuka katika miaka ya tisini na elfu mbili.
Kando ya serikali ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, Wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa, mataifa kadhaa ya magharibi yakiwemo Marekani na Ufaransa yamekuwa yakiituhumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23. Licha ya tuhuma hizo, serikali ya mjini Kigali imekuwa ikiyakanusha madai hayo.