1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC, Rwanda zakubaliana kusaka suluhisho

6 Novemba 2022

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda wamekubaliana kuharakisha juhudi za kuondosha hali ya wasiwasi na kuutatuwa mgogoro wao wa kisiasa unaotishia kuvunja mahusiano baina yao.

https://p.dw.com/p/4J7oy
DR Kongo, Protest in Goma
Picha: Michael Lunanga/AFP

Makubaliano hayo yamefikiwa kufuatia mazungumzo kati ya pande hizo mbili yaliyofanyika mjini Luanda siku ya Jumamosi (Novemba 5) chini ya upatanishi wa Rais João Lourenco wa Angola, ambaye amekuwa akiendesha kampeni ya kuyapatanisha mataifa hayo mawili jirani.

Mawaziri hao wamekutana wakati wasiwasi ukizidi kutokana na mashambulizi yanayofanywa na kundi la waaasi la M23 mashariki mwa Kongo, ambalo Kinshasa inasema linasaidiwa na Rwanda.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa siku ya Jumamosi inasema kwamba mazungumzo hayo "yataendeleza majadiliano ya kisiasa baina ya viongozi wa Kongo na Rwanda kama njia pekee ya kututuwa mzozo uliopo kati ya pande hizo mbili.

Mazungumzo hayo ni sehemu ya majadiliano yaliyoanza mnamo mwezi Julai ambapo nchi hizo mbili ziliahidi kukomesha uhasama na kuwaondosha wapiganaji wa M23 kutoka ndani ya ardhi ya Kongo.

Kuporomoka kwa mahusiano

Angola Luanda | Treffen der Präsidenten Kagame (L)  Lourenco (C) und Tshisekedi
Kutoka kulia: Rais Paul Kagame wa Rwanda, Joao Lourenco wa Angola na Felix Tshisekedi wa Kongo.Picha: JORGE NSIMBA/AFP

Mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi hizo yalifika pabaya mwezi uliopita, baada ya kundi la M23 kuanzisha mashambulizi mapya katika jimbo la Kivu Kaskazini na kuutwaa mji muhimu wa Kiwanja, hatua iliyoifanya Kongo kumfukuza balozi wa Rwanda nchini humo. 

Wiki iliyopita, maelfu ya raia walijiunga na maandamano ya kuipinga Rwanda katika mji wa Goma, ulio pia mashariki mwa Kongo. Kongo imekuwa ikiishutumu Rwanda kuliunga mkono kundi hilo lenye Watutsi wengi, na ambalo limekishambulia kituo cha jeshi la Kong karibu na mpaka wa Rwanda. Rwanda inakanusha tuhuma hizo.

Wakimbizi wa ndani wahitaji misaada Kongo

Kundi la M23 lilijizolea umaarufu na maeneo makubwa mashariki mwa Kongo mwaka 2012 kabla ya kushindwa vita na kuweka silaha chini kwa muongo mzima.

M23 yazidi kupata nguvu

DR Congo Anti Ruanda Protest M23 Rebels
Maandamano ya raia wa Kongo wakipinga kile wanachosema ni mkono wa Rwanda kwenye mashambulizi yanayofanywa na M23.Picha: Benjamin Kasembe/DW

Kujitokeza kwake tena hadharani mwaka huu kunatokana na kile linachodai ni kutokutekelezwa kwa ahadi ya kuwajumuisha wapiganaji wake kwenye jeshi, miongoni mwa malalamiko yake mengi.

Eneo la mashariki mwaKongo limekuwa kiini cha machafuko kwa takribani miongo mitatu sasa kutokana na kushamiri kwa makundi yenye silaha.

Kenya imetuma wanajeshi wake kuimarisha kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kinachojaribu kutuliza hali ya mambo. 

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mapigano kati ya jeshi la Kongo na waasi wa M23 yamepeleka watu 50,000 kukimbia makaazi yao tangu Oktoba, ambapo 12,000 wamekimbilia Uganda.