1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je chama cha MDC Zimbabwe kitaweza kumuondoa Mugabe madarakani?

Saumu Mwasimba2 Agosti 2007

Swali hilo linawatia wasiwasi wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa Zimbabwe kwani Kambi ya upinzani nchini humo ya chama cha MDC iliyogawika imeanza upya kufarakana

https://p.dw.com/p/CHA5
Kiongozi wa chama cha Movement for Democratic Change MDC Morgan Tsvangirai
Kiongozi wa chama cha Movement for Democratic Change MDC Morgan TsvangiraiPicha: AP

Hii inatokea miezi michache tu baada ya kambi hiyo ya chama cha MDC (movement for Democratic Change) kuahidi kwamba wataondoa tafauti zao na kushirikiana katika juhudi za kumuondoa madarakani rais Robert Mugabe katika uchaguzi wa mwaka ujao.

Baada ya wanachama wa MDC kula mkong’oto wa vikosi vya usalama nchini Zimbabwe mnamo mwezi Marchi viongozi wa makundi mawili yanayopinga ndani ya chama hicho waliahidi kwamba kamwe hawatothubutu tena kuyumbishwa katika harakati zao za kutaka kumng’oa bwana Mugabe Madarakani.

Lakini ahadi hiyo ilivunjika mwishoni mwa juma pale bwana Athur Mutambara ambaye anakundi la wafuasi wengi wabunge kutoka chama hicho kumdhrau kiongozi wa MDC Morgan Changirai na kumtaja kuwa mtu asiye na lolote wala chochote.

Kwa upande wake Changirai alimshutumu mpinzani wake bwana Mutambara kwa kupoteza mwelekeo na kuwabebesha lawama wasiokuwa walengwa.

Kutokana na mivutano hiyo ndani ya chama kikuu cha Upinzani MDC wachambuzi wa mambo wanaamini mshindi mkubwa ni rais Robert Mugabe anayetafuta kurudi tena ikulu kuongoza kipindi cha saba cha urais pindi mwakani wakati ambapo uchumi wa taifa hilo umeyeyuka mithili ya theluji juani huku Zimbabwe ikiziti kutengwa kidiplomasia.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa mjini Harare Takura Zhangazha anasema uhasama huu uliopo ndani ya chama cha MDC ni kama vile vita vya panzi na furaha milele humuendea kunguru.

Na hata rais Mugabe mwenyewe amekuwa akikumbusha mara kwa mara kwamba anaamini hakuna hata siku moja chama cha MDC kitaweza kufanikiwa kuingia ikulu

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Takura Zhangazha anaongeza kusema kwamba ni bahati mbaya kwa wanaMDC kulumbana wakati huu hasa wanapotaka kupigania nafasi ya kidemokrasia nchini Zimbabwe.

Mtazamo kama huo unachukuliwa na mwenyekiti wa baraza kuu la kitaifa la masuala ya Katiba Lovemore Madhuku.

Yeye anasema ni bayana kwamba rais Robert Mugabe ataendelea kuwepo madarakani na hii ni kutokana na tafauti za kibinafsi zilizoibuka tena ndani ya chama cha MDC,chama hicho kimekosa viongozi makini na madhubuti na baada ya uchaguzi wa mwaka ujao pana haja ya watu kuwa makini katika kuwa na upinzani uliona mshikamano na kuwachagua viongozi wapya wa upinzani.

Chama cha MDC kiligawika makundi mawili mwaka 2005 kutokana na suala la kuamua ikiwa chama hicho kisusie au kishiriki uchaguzi wa seneti ambao kwa mujibu wa bwana Changirai ulikuwa ni uharibifu wa fedha.

Tofauti ndani ya chama hicho zilionekana kupungua baada ya makundi yote mawili ya MDC kujikuta mashakani mikononi mwa serikali ya Mugabe na kupewa mkongoto mkali sana mwezi Marchi jambo ambalo liliwaleta pamoja na kuanza kuangaza mbele kuhusu kumuondoa madarakani Mugabe.

Lakini mwenye lake haachi mivutano imeibuka tena Mutambara anasema Morgan Changirai ni dhaifu na mtu mwenye shaka shaka nyingi ambaye hawezi kuyakubalia matakwa ya wazimbabwe wa kawaida kwa hiyo anawekea alama ya kuuliza ikiwa kweli anafaa kuongoza taifa.

Hivyo basi waziri wa zamani wa habari Jonathan Moyo ambaye amejitenga na chama tawala cha ZANU PF anautahadharisha upinzani akisema ni kosa kubwa kwa upinzani kukosa kutatua tofauti zao , hiyo itampa ushindi kwenye sahani bwana Robert Gabriel Mugabe.