1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jaribio la mauaji dhidi ya Trump lachunguzwa

Angela Mdungu
14 Julai 2024

Shirika la Ujasusi la Marekani linachunguza jaribio la mauaji lililomlenga Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.

https://p.dw.com/p/4iGeg
Donald Trump baada ya kujeruhiwa katika jaribio la kumuua
Walinzi wakimzingira Donald Trump baada ya mgombea huyo wa Urais wa Marekani kufyatuliwa risasi iliyomjeruhi sikioniPicha: REUTERS

Tukio hilo lilitokea Jumamosi wakati Trump alipokuwa akifanya mkutano wa hadhara katika jimbo la Pennsylvania. Mtu mmoja alifyatua risasi kadhaa na kumjeruhi sikioni Rais huyo wa zamani wa Marekani.     

Shirika la upelelezi la Marekani la FBI limesema mwanamume huyo aliyeuwawa  mara tu baada ya kufanya  shambulio hilo, ametambuliwa kuwa ni kijana Thomas Matthew Crooks mwenye miaka 20 na mkaazi wa jimbo la Pennsylvania. Uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo unaendelea.

Watu walioshuhudia tukio hilo wamesema walimuona mtu mwenye silaha kabla ya shambulio hilo na waliziarifu mamlaka. Hata hivyo polisi wamesema walipokea taarifa kadhaa za shughuli zenye kutia shaka, bila kufafanua zaidi. Mtu mmoja aliyekuwa katika mkutano huo aliuwawa katika shambulio hilo. Rais Joe Biden, amelilaani shambulio hilo dhidi ya Trump na kusema kuwa matukio ya aina hiyo hayana nafasi katika taifa hilo.