Biden: Niko sawa kiafya hivyo msiwe na hofu
13 Julai 2024Rais wa Marekani Joe Biden alirejea kwenye kampeni siku ya Ijumaa akiendelea kuwahakikishia wapiga kura na wanachama wa chama chake cha Democratic kuhusu kufaa kwake kuwa madarakani baada ya mkutano mkubwa wa waandishi habari kushindwa kuizima miito ya kumtaka ajiondoe kwenye kinyang'anyiro hicho.
Akiwa mjini Northvillle katika jimbo la Michigan, Biden amewahakikishia wafuasi wake kwamba yuko vizuri na kwamba ni lazima amshinde mpinzani wake Donald Trump katika uchaguzi wa nchi hiyo mwezi Novemba.
Soma zaidi. Kanda ya Indo Pasifiki na NATO wajiimarisha kukabiliana na vitisho vya usalama
Lakini kelele za wanachama wa Democratic zinazomtaka ajiondoe zinazidi kuongezaka, huku wabunge 19 wa chama chake wakimtaka waziwazi asigombee tena uchaguzi kufuatia kushindwa kwake vibaya katika mdahalo dhidi ya Trump mnamo Juni 27.
Akiwa kwenye mkutano wa jumuiya ya kujihami NATO uliofanyika wiki hii, Biden alikosea kwa kumuita makamu wake Kamala Harris , Makamu wa rais Trump na baadaye pia akamuita rais wa Ukraine Volodymir Zelensky kwa kumuita jina la rais Putin. Mfululizo wa matukio hayo unaongeza shinikizo juu ya uwezo wake wa kiakili ingawa yeye anasisitiza kuwa yuko sawa.