Waziri Mkuu wa Hungary Orban akutana na Trump huko Florida
12 Julai 2024Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban amekutana na rais wa zamani wa Marekani Donald Trump mjini Florida muda mfupi baada ya kuhudhuria mkutano wa kilele wa jumuiya ya kujihami ya NATO mjini Washington.
Orban ameweka picha yake na Trump katika mtandao wa kijamii wa X ikiwa na maandishi yaliyosema "mpango wa amani."
Orban amesema kwamba yeye na Trump wamejadiliana njia za kuleta amani na kudai kwamba Trump ataleta usuluhishi.
Soma pia: Waziri Mkuu wa Hungary , Rais Xi Jinping wakutana Beijing
Orban ameendelea kuwa na mahusiano mazuri na Trump tangu ushindi wa rais huyo wa zamani katika uchaguzi wa mwaka 2016.
Mara ya mwisho viongozi hao wawili kukutana ilikuwa mwezi Machi na baada ya hapo Orban akamuita Trump kama "rais wa amani" na Trump akamtaja Orban kama "kiongozi mzuri." Trump analenga kurudi White House kwa tiketi ya chama cha Rerpublican baada ya uchaguzi wa Novemba mwaka huu ambapo atakuwa anapambana na Joe Biden wa chama cha Democratic.